Msekwa afichua siri ya kuzaliwa Muungano

MWANASIASA mkongwe na Spika wa Bunge mstaafu, Pius Msekwa ameeleza namna uhusiano na ushirikiano wa kindugu baina ya viongozi waasisi wa muungano ulivyozaa Muungano wa Tanzanyika na Zanzibar.
Kupitia picha mjongeo iliyotolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira kuelekea miaka 61 ya Muungano, Msekwa alisema Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume walikuwa na uhusuano wa kirafiki na walikuwa wanashirikiana katika mambo mengi yaliyozaa muungano.
“Viongozi wa vyama viwili hivi chama cha Rais Karume (Abeid Aman Karume) Afro-Shiraz Party na chama cha Rais Nyerere (Julius Nyerere) TANU, viongozi wenyewe walikuwa wanafahamiana ni marafiki wanashirikiana katika mambo mengi.”
Alieleza namna uhusiano huo wa kirafiki baina ya Mwalimu Nyerere na Karume ulivyochochea ukaribu baina ya vyama vyao kwa kushirikiana katika shughuli mbalimbali za kijamii na kutembeleana.
“Undugu wa viongozi hawa ukafanya na undugu wa vyama kuwa ni mkubwa kwa maana viongozi kutembeleana kama kukiwa na shughuli za sikukuu wa upande ule (Zanzibar) wanakuja upande huu (Bara) wanashiriki, kulikuwa na uhusuano wa namna hiyo.”
Pia, Msekwa alieleza namna uhusiano wa kindugu ulikuwepo baina ya wananchi wa kawaida ulivyochangia muungano huo.
Alisema baadhi ya makabila, likiwemo kabila la Wanyamwezi walivutiwa na shughuli za kiuchumi hasa katika kilimo cha karafuu kilichosababisha wengi wao kuhamia katika visiwa vya Pemba na kuanzisha makazi ya kudumu.
“Wanyamwezi wengi walikuwa wanakwenda Pemba walikuwa wanachoma karafuu wakawa wakazi wa kule wakazaa na watoto hukohuko.”
Alieleza namna alivyokutana na wakazi wa Pemba waliotoka bara na wengi wao kuonesha kuwa wanafurahia muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Aprili 26, 2025 Tanzania inaadhimisha miaka 61 amnbayo ni zaidi ya nusu karne ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Tanzania ikishuhidia mafanikio makubwa katika nyanja zote za kijamii, kiuchumi na kisiasa.



