Msigwa aelezea kifo mwandishi wa TBC

MSEMAJI wa Serikali, Gerson Msigwa ameelezea kifo cha Mwandishi wa Habari wa TBC, Joachim Kapambe ambaye amesema alikuwa naye wakati wa kuupanda Mlima Kilimanjaro. Msigwa amesema amesikitishwa na taraifa hizo.
“Kapembe amefariki dunia kwa ajali ya baiskeli wakati akitoka katika kambi ya Kibo kuelekea kambi ya Horombo baada ya kupanda mlima hadi kufika kileleni kwa mafanikio.”
Amesema Kapambe hakupata madhara yoyote (mountain sickness) wakati wa kuupanda mlima huo na alifanya kazi yake ikiwemo kurekodi na kuhoji watu mbalimbali akiwemo Waziri, Nape Nnauye.
Msigwa ameeleza kuwa baada ya kufika kileleni mwa Kilimanjaro na kushuka watu wote walifika kambi ya Kibo ambako walipaswa kwenda kambi Horombo, wachache waliamua kutumia baiskeli badala ya kutembea kwa miguu akiwemo Kapembe.
“Bahati mbaya akiwa anateremka mteremko wa kutoka Kibo ndipo akapata ajali iliyosababisha apoteze maisha.” aliongeza Msigwa.
“Joachim Kapembe alikuwa Mwandishi wa Habari mahiri, aliyekuwa anajiamini, mchapakazi, mzalendo, mwenye nidhamu, muadilifu na aliyependa kufanya kazi kwa ushirikiano (Team Work) Natoa pole kwa Familia, Mkurugenzi Mkuu, Wafanyakazi wa TBC, Waandishi wa Habari wenzangu, ndugu jamaa na marafiki wote.” amemaliza Msigwa