Mtaalamu aeleza umri halisi ukomo wa hedhi

DAR ES SALAAM; Daktari bingwa wa magonjwa ya uzazi  na masuala ya wanawake Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk Lilian Mnabwiru, amesema kuna vipindi  vitatu anavipitia mwanamke anapofikia kikomo cha hedhi.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Dailynews Digital, Dk Lilian ambaye pia ni mbobezi katika masuala ya upandikizaji mimba,  amesema asilimia kubwa ya wanawake hukoma hedhi wakiwa na miaka 50 hadi 51.

“Kukoma kwa hedhi ni hali ya kawaida kwa mwanamke kulingana na vipindi vya maisha ukomo wa hedhi unaweza kutokea kwa wakati wowote, hali hii inatokea wakati miezi 12 mfululizo mwanamke hajaona siku zake au kwa lugha ninyingine kukosa hedhi kwa miezi hiyo mfululizo atakuwa amekoma,”ameeleza.

Dk Liliana anabainisha kuwa mara nyingi hali hiyo hutokea kuanzia miaka 40 mpaka 45 na kuna wanawake wanawahi kabisa miaka 35 na kuna baadhi wanachelewa  hadi umri wa miaka 60  mpaka 65.

Amebainisha kuwa kipindi kabla ya kuelekea kukoma hedhi kulingana na umri,  imegawanyika katika vipindi vitatu ambapo kipindi cha kwanza ni cha mpito kinachoanza na kuwa na mabadiliko, ambapo kichocheo kinaanza kushuka kwa kupunguza kasi na uwezo wa mayai kufanya kazi na kupungua taratibu.

“Baada ya kipindi hicho inaweza kuchukua miaka nane ndipo anakoma hedhi moja kwa moja. Katika kapindi hicho mabadiliko atakayoona kwenye hedhi ni kwenye mwezi mmoja anaona mara mbili au tatu wengine zinapungua siku kama 20 wengine zinazongezeka siku 30,” amesema na kuongeza kuwa wengine kama siku za kuwa hedhi ni saba zinabaki tatu hadi moja.

“Hali ya kukoma hedhi inasababishwa na  kushuka kwa kichochezo cha mwananmke kinachoitwa eostrojen kwa kiwango kikubwa, ambapo kinaposhuka husababisha mabadiliko mbalimbali katika mwili wa mwanamke,”amesisitiza.

Amesema ukomo wa hedhi huchangia kupungua kwa hisia za mwanamke. kwani homoni hiyo ndiyo inayomfanya aonekane mwanamke kama sauti nyororo,ngozi laini na muonekano wa kutofautishwa na mwanaume.

Aidha amesema kuwa mwingine anapungua siku za kuona hedhi kama ilikuwa siku saba inakuwa siku tatu au moja   na anapokuwa haoni kabisa kwa kipindi cha miezi 12 anakuwa amekoma hedhi.

Dk Lilian amefafanua kuwa katika kama  kipindi hicho  kitadumu kwa miezi 12 na baada ya hiyo miezi wanaangalia tena miezi mingine 12 kama hajapata hedhi ndio amekoma hedhi moja kwa moja.

Amesema sababu zingine za mwanamke  kukoma hedhi ni matatizo ya kiafya  ambayo yanahitaji kupata tiba zinazoweza kusababisha yeye kukoma hedhi.

“Mfano mwanamke anayekuwa na shida ya uzazi au shida katika mfumo wa uzazi labda anakuwa na matatizo kama uvimbe na mambo kama hayo yanayopelekea upasuaji wa kuondoa kizazi  na anapotolewa kizazi hawezi tena kuona hedhi.

Amesema  wengine wanaosumbuliwa na maradhi kama kansa na kusababisha tiba mbalimbali kama tiba ya mionzi na dawa za kemikali zinaweza kukomesha hedhi.

“Kuna ile inayotokana na asili kulingana na umri na kuna ile inayotokana na matatizo kama hayo kulingana na tiba anayopata lakini pia mwanamke anapokuwa mjamzito anaweza asione siku zake kwasababu ya ujauzito,”ameeleza.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button