Mtanzania aliyehusika mchoro tamasha kutawazwa Mfalme Charles III

KAMA kuna watu waliofanikiwa kuuza nchi zao kimataifa ni Shafina Jaffer, Mtanzania aliyeipeperusha vyema bendera ya nchi yake ughaibuni kutokana na umahiri wake katika taaluma yake ya uchoraji.

Ni miongoni mwa wanafunzi waliojumuika pamoja kutoka Chuo cha Sanaa cha Royal (Royal College of Arts-RCA) kilichopo London, Uingereza kuunda mchoro maalumu kwa ajili ya tamasha la kutawazwa kwa Mfalme Charles III na Malkia Camilla, hivi karibuni.

Shafina aliyehitimu stashahada ya uzamili katika uchoraji katika chuo hicho aliifanya Tanzania kung’aa kimataifa wakati mchoro wake ulipochaguliwa kutoka kwa mawasilisho zaidi ya 100 ya Ikulu na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), ili kujumuishwa katika kutawazwa kwa Mfalme Charles III.

Tamasha hilo lilifanyika Mei 7, mwaka huu katika uwanja wa Windsor Castle.

Mchoro wa Shafina ulioneshwa kwenye runinga kubwa iliyokuwa juu ya jukwaa na kwa nyuma eneo kubwa la Mashariki la Jumba la Windsor lilioneshwa vivyo hivyo na kufanya mlipuko wa shangwe.

Uchoraji wake uliunda mandhari ya uigizaji wa Romeo & Juliet ambayo iliunganisha muziki, dansi, sanaa na ukumbi wa michezo.

Ilitazamwa na mamilioni ya watu huku ikitoa mandhari nzuri ya anga ya usiku yenye nyota wakati wa mchezo wa moja kwa moja wa Shakespeare’s Romeo na Julie.

Michoro hiyo imeoneshwa kwa wageni 20,000 na kurushwa moja kwa moja kwa nchi 100 duniani kupitia BBC.

Michoro ya rangi za mafuta iliyonakishiwa na Msanii Mtanzania Shafina Jaffer ikiwa ni sehemu kazi ya sanaa aliyopata heshima ya kupamba katika Kasiri ya Buckingham katika sherehe ya kusimikwa Mfalme Charles wa III na mkewe Malkia Camilla iliyofanyikia jijini London, Uingereza hivi karibuni.

Taswira ziliunda mandhari ya kupendeza ikisindikizwa na wimbo uitwao ‘Mahali Pengine’ kutoka West Side Story katika onesho lililowashirikisha wasanii, Ncuti Gatwa na Mei Mac.

RCA kilifanya kazi na Chuo cha Royal cha Muziki, Royal Ballet, Royal Opera na Kampuni ya Royal Shakespear’s kwa mara ya kwanza kuzalisha ushirikiano huo wa kipekee wa ubunifu unaochanganya sanaa, muziki, dansi na kumbi za michezo kwa kuheshimu Ufalme wa Uingereza na watu wake.

Chuo hicho ni miongoni mwa vyuo vikongwe, kilianzishwa mwaka 1837 na ni chuo kikuu cha sanaa na ubunifu kinachoongoza duniani kwa ujuzi wa umahiri kinachopokea watu kutoka pande zote duniani.

Hakijapewa jina la Royal makusudi badi ni chuo chenye heshima ya Kifalme kinachotumiwa na familia ya Kifalme miaka na miaka.

Matokeo ya ubunifu wa kisanii ya Shafina yanatokana na maswali yake ya msingi kuhusu hali ya binadamu, vifo na ontolojia zilizobeba mustakabali wa maisha ya mwanadamu na mapito yake.

Sherehe, furaha na kucheza kupitia ulimwengu ni hisia zilizopo katika kazi yake ambayo ilichaguliwa kwa ajili ya sherehe hizo za Mfalme Charles wa III.

Mafunzo yake katika RCA na Shule ya Sanaa ya Jadi ya Princess yanatoa msukumo wa mchanganyiko unaoonesha mbinu za kitamaduni za urithi wake wa Kiafrika na utayari.

Katika uchoraji wa Kutawazwa Mfalme, uwepo wa nyota kubwa katika sehemu ya mchoro ulionakshiwa kwenye hafla hiyo na unatoa ishara ya nafasi ya kibinadamu katika ulimwengu.

Michoro yake yenye viwango vya hali ya juu inadhihirisha pia uwezo wake wa uelewa. Ni msikivu na mtii kwa uongozi, mwenye tamanio la kujifunza kila wakati kwa faida yake, familia na jamii kwa ujumla.

Habari Zifananazo

Back to top button