Mtwara wamuenzi Nyerere kuhamasisha uchaguzi

SERIKALI ya Mkoa wa Mtwara kwa kushirikia na wananchi mkoani humo imefanya matembezi ya kumbukizi ya miaka 25 ya kumuenzi Hayati Baba wa Taifa Julius Kambarage Nyerere pamoja na kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu uchaguzi wa serikali za mitaa.

Akizungumza leo baada ya matembezi hayo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Patrick Sawala amesema siku hiyo ni muhimu kwao kwasababu wanaenda kutekeleza haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi wa serikali za mitaa.

Amesema anatambua wengi wao tayari wameshajiandikisha katika daftari la mpiga kura lakini kwa wale ambao bado hawajajiandikisha ametoa rai wakajiandikishe ili wasikose haki yao ya kikatiba kuelekea uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Novemba 27,2024.

Advertisement

Hata hivyo kila mwenye sifa za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwenye uchaguzi huo aende akachukue fomu ya kugombea ili agombee haki yake.

“Vijana ni taifa la leo na la kesho, msiache nafasi hii mkagombee, akina mama mkagombee lakini pia wakati wa kampeni ni wakati mzuri wa kwenda kuwasikiliza wagombea na kuwapima ili itakapofika tarehe 27/ 10/ 2024 ya uchaguzi tukachague viongozi wiliyo bora,”amesema Sawala

Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara, Bahati Geuzye amesema uchaguzi huo utaongozwa na kanuni za uchaguzi wa viongozi wa mamlaka ya viongozi wa serikali za mitaa ngazi ya kijiji, vijiji, vitongoji na miata katika mamlaka za wilaya na miji.

Aidha matembezi hayo ni ya amani ambapo miomgoni mwa wananchi waliyoshiriki matembezi hayo wakiwemo waendesha bodaboda.

Katibu Msaidizi wa Chama cha Waendesha boda boda mkoani humo, Mshamu Ally amesema ataendelea kuwahamasisha wanachama wenzake na wananchi wengine kwenye maeneo yao ili washiriki kikamifu uchaguzi huo.

“Lakini kwa sehemu kubwa tumeshahamasisha ndio mana unaona hapa leo sisi bodaboda tumeshiriki zaidi ya bodaboda 500 katika matembezi haya na bado tutaendelea kuhamasishana zaidi”amesema Mshamu