Muhimbili wapokea vifaa matibabu ya macho

HOSPITALI ya Taifa ya Muhimbili imepokea vifaa vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 23 kwa ajili ya kusaidia matibabu ya macho sambamba na mafunzo ya upasuaji wa mtoto wa jicho kwa njia ya tundu dogo.
Vifaa hivyo vimetolewa na taasisi ya Vision Care yenye makao makuu nchini Korea Kusini na Marekani, ambapo taasisi hiyo ipo katika utekelezaji wa kupambana na magonjwa ya macho pamoja na kupika wataalamu mbalimbali kutoka kila kona ya dunia watakaosaidia katika harakati za kupambana na magonjwa hayo.
Mkurugenzi wa taasisi hiyo nchini Tanzania, Jieun Park amesema mbali na kukabidhi vifaa vitakavyosaidia kwenye matibabu ya magonjwa ya macho wanalenga pia kuongeza idadi ya wataalamu barani Afrika hususani Tanzania.
“Tupo katika mpango wa kupambania afya ya macho, taasisi yetu inafanya kazi katika nchi nyingi Afrika, tunataka kuacha ujuzi wetu katika maneneo mbalimbali ndio maana tutaongeza idadi ya madaktari bingwa,” amesema Jieun Park.
Daktari bingwa wa macho kutoka hospitali hiyo, Dk Joachim Kilemile amesema ujio wa mafunzo pamoja na vifaa hivyo ni neema kubwa, kwani vitasaidia kupunguza muda wa matibabu ya wagonjwa wa macho.
“Mashine kama hizi zitasaidia kujua ukubwa wa kioo ambacho mgonjwa anatakiwa kuwekewa baada ya upasuaji, lakini pia hata kupunguza muda wa matibabu,” amesema Kilemile.
Taasisi hiyo imeandaa mafunzo ya siku tano yaliyoanza leo Julai 3 na yatafika tamati Jualai 7, 2023 katika Hospitali ya Muhimbili, ambapo madaktari bingwa pamoja na waaguzi watashiriki mafunzo hayo ili kufikia azma yao ya kuongeza wataalamu ulimwenguni kote.