Muhimbili yapeleka msaada Hanang
MANYARA: Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imepeleka msaada wa dawa na vifaa tiba vyenye thamani ya Sh milioni 38 ili kusaidia jitihada za utoaji huduma katika mji mdogo wa Katesh wilayani Hanang, mkoani Manyara.
Hivi karibuni eneo hilo la Katesh lilikumbwa na maafa ya mafuriko yaliyosababisha maporomoko ya udongo kutoka Mlima Hanang na kusababisha madhara ikiwemo vifo, majeruhi pamoja na upotevu wa mali na uharibifu wa miundombinu.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Mkuu wa Idara ya Famasi, Mfamasia, Nelson Faustine amesema pamoja na msaada huo, hospitali imetuma Msaikolojia Tiba kwenda kuungana na timu za watalam mbalimbali walioko wilayani Hanang mkoani Manyara wanaotoa huduma kwa waathirika wa mafuriko hayo.
Amesema, hatua hii ni kuitikia wito wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ambaye ameagiza kupelekwa watalaam wa saikolojia kuzungumza na wananchi waliopata mfadhaiko kutokana na tukio hilo ili waweze kurejea katika hali ya kawaida.