Muhimbili yapokea taulo za watoto wachanga

DAR ES SALAAM: Hospitali ya Taifa Muhimbili imekabidhiwa msaada wa taulo za watoto wachanga aina ya Softcare zenye thamani ya  Sh milioni 35 kutoka kampuni ya DOWEICARE ili kusaidia watoto waliozaliwa na watakaozaliwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia sasa.

Akipokea msaada huo kwa niaba ya Serikali, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ameipongeza DOWEICARE kwa mchango huo ambao utasaidia kina mama na watoto wao hasa wasio na uwezo wa kumudu kununua taulo hizo mara tu wanapojaliwa kupata baraka za watoto.

“ Mmeonesha kujali kwani taulo hizi zitasaidia katika kutunza na kuandaa afya ya mtoto ambaye siku za usoni atakuwa kiongozi mwenye mawazo chanya na akili njema itakayotumika katika kuliongoza taifa letu, ” amesema Chalamila na kuongeza

“Mara nyingi tumekuwa tukitoa msaada kwa watu wazima na kusahau kuwa watoto ni watu muhimu katika jamii hasa katika kuandaa taifa imara na bora lenye maendeleo makubwa,” amesema.

Akipokea msaada huo Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi ameishukuru kampuni hiyo na kuwaomba kuendelea kuunga mkono hospitali kutokana na kuhudumia wagonjwa wengi na wenye vipato tofauti.

“Tunajua nyie niwatengenezaji wa bidhaa muhimu ambazo tunahitaji zaidi katika kuwahudumia watoto hivyo ombi letu kwenu ni kuwa tunaomba hapo baadaye mtuuzie bidhaa hizi kwa bei ya punguzo kwani kufanya hivyo mtakuwa mmewasaidia watoto wachanga wanaozaliwa na kuhudumiwa hospitalini hapa,” amesema Prof. Mohamed.

Akikabidhi msaada huo Mkurugenzi Mtendaji wa DOWEICARE Victor Zhang amesema  wanatambua mchango mkubwa unaotolewa na hospitali hiyo hivyo wataendelea kushirikiana ili kuboresha huduma za afya katika maeneo kadhaa.

Habari Zifananazo

Back to top button