Muhimbili yavuna mbavu, yatengeneza taya

DAR ES SALAAM: HOSPITALI ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa mara ya kwanza imefanya upasuaji wa kutoa mfupa kwenye ubavu wa binadamu na kukiweka kama kiungo cha taya la chini ya fuvu.

Akizingumza leo Februari 28, 2024 baada ya upasuaji huo, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Uso na Taya, Arnold Augustino amesema, mgonjwa huyo amefanyiwa upasuaji wa kuondoa taya lote la kulia lililoathiriwa na uvimbe na hivyo kumtengenezea taya jipya kwa kuchukua mfupa kutoka kwenye ubavu ambapo mfupa huo umepandikizwa kwenye kiungio cha taya.

Amesema kuwa mifupa mingine imechukuliwa kutoka kwenye nyonga pande zote mbili ili kuunganishwa na mfupa uliotolewa kwenye ubavu kuwezesha kutengenezwa kwa taya sawasawa na taya lake la awali na kisha kuunganishwa na kipandikizi cha chuma maalum kutengeneza sehemu ya taya iliyoharibika kwa ugonjwa.

“Baada ya upasuaji huu tunategemea mgonjwa ataendelea kula na kutafuna kama kawaida kwani tutamuwekea meno bandia kwenye mfupa wa taya tulioutengeneza,”amesema.

Aidha, amesema  kuwa mgonjwa huyo amefanyiwa upasuaji aina tatu tofauti kwa wakati mmoja, wa kutoa kipande cha mfupa kwenye ubavu, wa pili ni kutoa mifupa kwenye nyonga zote mbili na wa tatu ni kuondoa uvimbe ambapo umechukua saa saba.

Amesema upasuaji huo umeshirikisha timu watalaam wa MNH madaktari bingwa wa taya na uso watano, wataalamu usingizi na ganzi wawili, manesi wa upasuaji watatu, na wataalamu wengine waliokuwepo ni pamoja madaktari wanaosomea ubingwa wa kupasua mataya na uso.

Habari Zifananazo

Back to top button