Muhtasari wa majadiliano kuhusu maboresho ya kodi
KADRI Tanzania inavyoendelea na harakati za maboresho ya kodi, ni muhimu kufanya tafakuri kuhusu mada kuu zilizojadiliwa katika mfululizo wa makala haya.
Mjadala huu wa mwisho utatumika kama muhtasari wa kina wa masuala muhimu, maoni na masuala ya sera.
Makala haya leo yanalenga kuwapa wasomaji uelewa wa pamoja wa changamoto, fursa, njia na mwelekeo sahihi wa
mazingira ya kodi ya Tanzania.
Katika kuhitimisha mjadala huu, tunawaachia wasomaji nafasi ya kutafakari zaidi na kujihusisha na mawazo
yaliyotolewa, kuhimiza mazungumzo endelevu na kutafakari mustakabali wa sera ya kodi
nchini.
Kifungu cha 1 hadi 10
Katika vifungu kumi, mfululizo wa makala haya umejadili maboresho ya mfumo wa kodi wa Tanzania yaani namna
ulivyokuwa, changamoto zilizopo sasa na maboresho yanayounda mustakbali wake.
Kuanzia Kifungu cha 1 hadi Kifungu cha 10 tumeona namna kulivyotokea mabadiliko ya kodi nchini Tanzania kutoka
kuwa chombo cha kikoloni cha kudhibiti uchumi hadi kuwa muundo wa kisasa wa fedha unaolenga kukuza uwekezaji na uendelevu.
Katika mijadala ya mwanzo, tuliangalia misingi ya kihistoria ya sera za kodi za Tanzania. Kifungu cha 1 kilitupitisha
katika zama za ukoloni wakati kodi ya moja kwa moja kama vile kodi ya nyumba iliyoundwa si tu kwamba ilikuwa
kwa ajili ya mapato, bali pia kuwezesha harakati za watu kutoka sehemu moja hadi nyingine ili kuajiriwa katika
uchumi unaotegemea fedha taslimu.
Katika Kifungu cha 2 na Kifungu cha 3, tumeona namna maboresho yaliyofanyika baada ya uhuru yalivyotaka
kuweka udhibiti, ukusanyaji wa kodi, ukaguzi na rufaa kwa nchi kuwa chini ya taasisi moja kwa kutegemea zaidi
ushuru wa mazao ya kilimo na mashirika ya serikali.
Mabadiliko kuelekea ukombozi wa kiuchumi katika miaka ya 1990, kama yalivyojadiliwa katika Kifungu cha 4 na 5,
yalianzisha hatua kama vile Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na upunguzaji wa kodi ya mashirika au kampuni ili
kuvutia uwekezaji.
Kimsingi, maboresho hayo pia yalibainisha udhaifu wa kimfumo hasa mchango mdogo wa sekta isiyo rasmi licha ya
kuwa inachangia zaidi ya asilimia 50 ya Pato la Taifa. Tulipoingia katika Kifungu cha 6 na cha 7, tulijikita katika
nafasi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika uboreshaji wa ukusanyaji wa kodi hususani kupitia juhudi za
kuleta mabadiliko ya kidijiti.
Matumizi ya vifaa vya fedha vya kielektroniki (EFDs) na mifumo ya uwasilishaji taarifa kimtandao yalionesha
maendeleo ingawa kama ilivyobainishwa katika Kifungu cha 8, mfumo huo bado umegawanyika na kulemewa na
vyombo vingi vya kukusanya kodi vinavyosababisha kuwapo mwingiliano wa masuala ya kodi uwepo wa gharama
kubwa za utekelezaji wa taratibu, kanuni na sheria za kodi kwa biashara.
Kodi za mashirika zilizozungumzwa katika Kifungu cha 9, bado ni suala la tata
Aidha, kiwango sawa cha kodi cha asilimia 30 kwa kampuni/mashirika Tanzania kinaleta changamoto kwa biashara ndogo na za kati huku kikiruhusu mashirika ya kimataifa kudhibiti motisha na misamaha ili kupunguza mzigo wa kodi.
Tulitazama pia namna nchi kama Mauritius na Singapore zilivyotumia vivutio/motisha za kodi kwa sekta mahususi
kuchochea uvumbuzi na ukuaji wa uchumi; maarifa hayo yanaweza kuonesha mtazamo wa Tanzania. Aidha, Kifungu cha 10 kinaonesha mabadiliko ya utegemezi wa mapato kwa kodi zisizo za moja kwa moja kama vile Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), mwelekeo unaoathiri zaidi watu wa kipato cha chini.
Suala la kodi binafsi pia limejadiliwa pamoja na nafasi ya masoko ya mitaji ya Tanzania sambamba na haja kubwa ya kuwapo ushirikiano wa kimataifa katika utekelezaji wa masuala ya kodi.

Namna Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) linavyonufaika kutokana na vivutio vya kodi pamoja na namna mifumo ya kimataifa ukiwamo ubadilishanaji wa taarifa kielektroniki (AEOI) inavyoweza kusaidia Tanzania kufuatilia utajiri wake na kukabili ukwepaji kodi, ni masuala ambayo pia yalitazamwa kwa kina.
Mjadala unapohitimishwa, hapa kuna jambo moja lililo wazi kwamba, njia ya Tanzania kuelekea maboresho ya kodi lazima iwe ya kimkakati, shirikishi na inayoongozwa na teknolojia.
Kimsingi, suala la kupanua wigo wa vyanzo vya kodi kwa kurasimisha sekta isiyo rasmi, kurahisisha ukusanyaji wa kodi pamoja na kuoanisha sera za kodi na sekta muhimu ni lazima kwa manufaa ya utulivu wa muda mrefu.
Aidha, maboresho lazima yatoe kipaumbele katika usawa na kuhakikisha ulipaji kodi unasaidia ukuaji wa uchumi huku ukiwa wa usawa kwa biashara na watu binafsi. Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi inawakilisha hatua
muhimu kuunganisha mbinu bora, ushirikishwaji wadau pamoja na sera zinazoongozwa na data.
Kadiri Tanzania inavyoendelea kuboresha mfumo wa kodi, mafunzo yanayotokana na vifungu hivi kumi yatatumika kama msingi wa kuunda mfumo bora zaidi, uwazi na mfumo wa kodi wenye usawa huku ukichochea maendeleo
endelevu na ustawi wa taifa.
Kifungu cha 11 hadi Kifungu cha 17
Kuanzia Kifungu cha 11 hadi Kifungu cha 17, wadau wamejadili mabadiliko ya mfumo wa kodi nchini wakijikita katika haja kubwa ya kuwa na ufanisi, kutekeleza masuala ya kodi na mkakati wa maboresho.
Mijadala iliyotokana na maarifa ya awali ilitokana na mapendekezo ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na mbinu bora za kimataifa kuhimiza uwiano kati ya uzalishaji wa mapato na ukuaji wa uchumi.
IMF inasisitiza kuwa, usimamizi wa kodi lazima ubadilike, mifumo ya kisasa ya ukusanyaji kodi haina budi kuchukua nafasi ya mifumo iliyopitwa na wakati na misamaha ya kodi ambayo kwa muda mrefu imekuwa chanzo cha uvujaji wa mapato. Lazima tathmini mpya ifanyike. Mafanikio katika juhudi hizi yanategemea hasa uwezo wa Tanzania kurahisisha utekelezaji, kupunguza mizigo ya kiusimamizi na kuunganisha teknolojia ili kuchochea
ulipaji kodi.
Kipengele muhimu katika ajenda hii ya maboresho iliyojadiliwa katika Kifungu cha 13 kilikuwa kuanzishwa kwa
Mkakati wa Mapato ya Muda wa Kati (MTRS) kuhakikisha kuna uendelevu katika sera za fedha. Kupitia mbinu ya kupanga kodi, MTRS inalenga kuziba mianya, kurahisisha kanuni za kodi na kuimarisha utekelezaji wa sheria za kodi.
Mikakati kama hiyo imeonesha namna upangaji mapato wa muda mrefu unavyoongeza utabiri sahihi na uwazi katika ukusanyaji wa kodi katika nchi za Papua New Guinea na Senegal. Uimarishaji wa usimamizi wa kodi bado ni lengo kuu na IMF inasisitiza kupitishwa kwa zana za kidijiti, kutoa mafunzo kwa maofisa wa kodi pamoja na kutunga sheria zinazorahisisha kanuni za kodi.
Masomo yaliyopatikana kutoka Burkina Faso na Georgia yanaonesha kuwa, kurahisisha miundo ya kodi huku hatua za kutekeleza sheria na masuala ya kodi zikiimarishwa kunaweza kukuza kwa kiasi kikubwa ukusanyaji wa mapato bila kulemea walipa kodi.
Mada nyingine muhimu ilikuwa katika Kifungu cha 1 kuhusu Makubaliano ya Kuepusha Kodi Maradufu (DTAs)
na nafasi yake katika kuvutia uwekezaji kutoka nje hususani katika sekta kama ujenzi, madini na fedha.
Mikataba hii inawalinda wawekezaji wasitozwe mara mbili au zaidi, hivyo kuifanya Tanzania kivutio zaidi cha
biashara ya mipakani. Hata hivyo, bado changamoto zipo katika uoanishaji wa majukumu ya mkataba na
vipaumbele vya kodi ya ndani.
Uzembe kiutawala, utekelezaji usio thabiti pamoja na matumizi mabaya ya mikataba kupitia uhamishaji faida kutoka nchi zenye kodi ya juu kwenda maeneo yenye kodi nafuu ni kati ya mambo unayoendelea kuzua hofu.
Mfano mzuri ni mgogoro wa kodi ya Bharti Airtel ulionesha changamoto kubwa katika usimamizi wa kodi kuvuka
mipaka huku Mradi wa Bandari ya Bagamoyo ukiibua maswali ya kina kuhusu utegemezi wa Tanzania katika uwekezaji kutoka nje.
Nchi inapofanya kazi kuvutia wawekezaji, lazima pia ilinde maslahi ya taifa kuhakikisha sera za kodi zinachangia
uendelevu wa uchumi wa muda mrefu. Nafasi ya biashara ndogo na za kati imezingatiwa katika Kifungu cha 15 kinachosisitiza mchango wa biashara hizo wa zaidi ya asilimia 35 katika Pato la Taifa na changamoto za kimuundo zinazoikabili mfumo wa kodi.
Biashara nyingi zinaona kodi kama adhabu na gharama kubwa inayokatisha tamaa urasimishaji na kukwamisha
ufikiaji wa mkopo na msaada wa serikali. Georgia na Kenya ni mifano inayoonesha namna taratibu za kodi zilizorahisishwa, msamaha wa kodi kwa muda maalumu na programu za ulipaji kodi kwa awamu zilivyohamasisha urasimishaji wa biashara ndogo huku ikiimarisha ukusanyaji mapato.
Ufumbuzi wa kulipa kodi kidigiti kwa kutumia simu umeibuka kama njia ya kuboresha ulipaji kodi hasa kwa biashara katika maeneo ya vijijini, kupunguza urasimu na kufanya ulipaji kodi kuwa rahisi na unaofikiwa zaidi.
Kifungu cha 16 kimeangalia changamoto inayoendelea ya kurasimisha sekta isiyo rasmi ambayo ni hatua muhimu katika kupanua wigo wa vyanzo vya kodi Tanzania.
Hii ni kwa kuwa wafanyabiashara wengi wadogo wako nje ya mifumo rasmi ya kodi kutokana na ukiritimba, kutokujua masuala ya fedha na hofu ya kutozwa kodi kupita kiasi. Nchi kama Ethiopia na Rwanda zimeonesha kuwa
ulipaji kodi kwa awamu, motisha za kifedha na mifano ya kodi maalumu kwa sekta mahususi inaweza kuhamaisha
biashara zisizo rasmi kuingia katika uchumi rasmi.
Suluhisho la masuala ya kodi kidijiti linatoa fursa ya kuziba pengo baina ya wafanyabiashara wasio rasmi na
mamlaka ya kodi ili kuhakikisha kuna mfumo jumuishi wa kodi na kuongeza ufanisi zaidi. Mjadala wa mwisho katika Kifungu cha 17 ulijikita kutazama Tanzania inavyoweza kuweka mazingira rafiki ya kodi ya biashara huku ikidumisha uendelevu wa mapato.
Mbinu iliyopo ya kiwango kimoja cha kodi kwa wote haizingatii mahitaji ya kipekee ya sekta mahususi kama kilimo,
teknolojia na (uzalishaji) viwanda.
Sera madhubuti zaidi ya kodi kama vile vivutio vinavyohusu sekta mahususi, mifumo maalumu ya kodi kwa biashara mpya pamoja na ratiba za malipo zinazohusiana na mtiririko wa pesa za biashara zinaweza kuchochea ukuaji wa sekta na kuhakikisha kuna uthabiti katika ukusanyaji wa mapato.
Nchi kama India na Kenya zimefanikiwa kutekeleza hatua hizo na kuonesha kuwa, sera bora na madhubuti za kodi
zinaweza kuchochea uwekezaji na uvumbuzi. Suala lingine muhimu ni usimamizi katika utekelezaji, huku wafanyabiashara wengi wadogo na wa kati wakihisi kutengwa na mbinu ya matumizi ya adhabu.
Kugeukia mbinu saidizi zaidi inayojumuisha programu za elimu ya kodi na mabaraza ya ushauri, kunaweza kujenga
upya imani ya umma katika mfumo wa kodi. Mifano ni katika nchi za Australia na Afrika Kusini ambapo kujitokeza kwa hiari na motisha katika ulipaji kodi kumeboresha ushiriki katika masuala ya kodi kukionesha namna usimamizi bora unavyoweza kuwa na ufanisi zaidi kuliko adhabu.
Wakati Tanzania inaendelea na safari yake ya maboresho ya kodi, hatua za kimkakati, za awamu na za kukabiliana ni muhimu kuhakikisha kuna mafanikio ya muda mrefu. Hatua za kwanza zinahusisha ukusanyaji wa kodi kidigiti, kupunguza gharama za utekelezaji wa sheria za kodi na kuongeza uwazi kwa umma.
Kwa muda wa kati, Tanzania haina budi kuoanisha mikataba ya kuzuia ulipaji kodi maradufu (DTA) na malengo ya kiuchumi ya kitaifa, kuunganisha sera za kodi na mikakati zaidi ya maendeleo pamoja na kuunda motisha
zinazosaidia biashara za ndani na wawekezaji wa kigeni.
Kwa muda mrefu, lengo ni kukuza mfumo wa kodi unaotabirika, jumuishi na ambao ni rafiki wa kibiashara
unaoendeleza uwekezaji huku ukidumisha haki na ufanisi.
Kwa kutumia maboresho ya kimuundo yanayoongozwa na teknolojia na ujumuishi, Tanzania inaweza kujenga mfumo wa kodi ambao si tu kwamba unasaidia uimara wa kiuchumi na kimaendeleo, bali pia unahakikisha kuna uwajibikaji na haki.
Mafanikio katika maboresho haya yatategemea utashi wa kisiasa, ushiriki wa wadau na makabiliano endelevu ya uchumi inayobadilika. Kadiri nchi inavyosonga mbele, uwezo wake wa kuwianisha vivutio vya uwekezaji na nidhamu ya fedha utaamua kama mfumo wake wa kodi unaweza kutumika kuchochea ukuaji wa muda mrefu.
Kifungu cha 18 hadi Kifungu cha 22
Kuanzia Kifungu cha 18 hadi Kifungu cha 22, tulifikia sura za mwisho katika uchunguzi wa mfumo unaobadilika wa kodi Tanzania tukijikita katika changamoto za kimuundo na kiutawala zinazokwamisha na kuzuia ufanisi, ulipaji kodi na ukuaji wa uchumi.
Mijadala hii ilijikita kutafakari namna Tanzania inavyoweza kuunda mfumo wa kodi ambao si tu kwamba unazalisha mapato, bali pia unakuza uaminifu, unahamasisha ulipaji kodi kwa hiari na unaosaidia maendeleo ya muda mrefu ya
taifa.
Moja ya vikwazo vinavyoendelea vilivyojadiliwa katika Kifungu cha 18, ni mgawanyiko wa mamlaka za kukusanya kodi. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inafanya kazi pamoja na mamlaka za serikali za mitaa na taasisi za udhibiti, kila moja ikiweka mchanganyiko wa kodi, tozo na ada.
Muundo huu unaoingiliana unasababisha mkanganyiko miongoni mwa walipakodi, unakatisha tamaa ulipaji kodi
kwa hiari na kusababisha uwiano wa kodi kwa Pato la Taifa wa asilimia 11.9 ambao ni chini ya wastani wa Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara ambao ni asilimia 16.
Baadhi ya nchi ikiwamo Rwanda, zimefanikiwa kurahisisha usimamizi wa kodi na kufanya ukusanyaji kodi kuwa
chini ya chombo kimoja kuongeza ufanisi na kuunda mazingira rafiki zaidi ya biashara. Kama Tanzania itafuata mfano huo, itaongeza ukusanyaji wa kodi huku pia ikipunguza mzigo wa kodi kwa wafanyabiashara wadogo.
Kimsingi, suala ushirikishwaji wa umma katika sera ya kodi lililojadiliwa katika Kifungu cha 19, bado ni pengo kubwa katika mchakato wa maboresho. Nchini Tanzania, mara nyingi mipango ya maboresho ya kodi imekuwa ‘ikitoka juu kuja chini’ huku ikihusisha mchango mdogo kutoka kwa wafanyabiashara au wananchi, hususani walio katika sekta isiyo rasmi.
Hili huondoa hali ya kutoaminiana kwa umma na kufanya ulipaji kodi kuwa mgumu zaidi. Katika nchi kama Uganda
na Kenya ukosefu wa mashauriano ya sera ya kodi umesababisha upinzani mkubwa wa umma na kushindwa kwa sera na hivyo, kusisitiza umuhimu wa kushirikisha umma kupitia kamati za wadau, kampeni katika vyombo vya habari na mipango ya kufikia umma kidijiti.
Kuimarisha uwazi katika uundaji wa sera ya kodi kunaweza kuboresha imani ya walipa kodi na kuchochea ulipaji kodi. Kama Kifungu cha 20 kinavyobainisha, ulipaji kodi ni moja ya changamoto kubwa nchini Tanzania. Biashara hususani ndogo na za kati zimeendelea kutokuwa rasmi ili kuepuka michakato mgumu wa usajili, utekelezaji
usiotabirika pamoja na urasimu wa kupindukia.
Mtazamo wa kodi kama adhabu badala ya maendeleo unaendelea kukatisha ushiriki. Urahisishaji ni jambo la msingi kwa kuunganisha suluhu za malipo ya kodi kwa simu, vivutio vya kodi kwa sekta mahususi, na michakato ya usajili wa kidijiti ni mambo yanayoweza kuboresha kwa kiasi kikubwa viwango vya ulipaji kodi.
Estonia na Rwanda zimeonesha namna mfumo wa kodi wa kidijiti unavyopunguza rushwa na kuongeza ufanisi, huku ukaguzi wa kodi unaoongozwa akili mnemba (AI) na ufuatiliaji wa kielektroniki ukichukua nafasi kubwa kurahisisha ukusanyaji wa mapato.
Utekelezaji wa ufumbuzi kama huo nchini Tanzania unaweza kufanya mfumo wa kodi kuwa wa kisasa na hivyo,
kupunguza uvujaji wa mapato. Changamoto nyingine kubwa iliyojadiliwa katika Kifungu cha 21, ni mwingiliano
baina ya ukusanyaji wa kodi na matumizi ya serikali.
Kukosekana kwa uwazi katika matumizi ya fedha za umma kumeondoa imani katika mfumo huo na kufanya ulipaji kodi kuwa mgumu. Aidha, usimamizi mbovu wa fedha umesababisha ufinyu wa bajeti, utoaji wa huduma kwa umma usio na tija pamoja na kukua kwa deni la taifa.
Brazili na Ujerumani ni nchi zilizotekeleza kwa ufanisi mkubwa utungaji wa bajeti kadiri ya utendaji na sheria kali zaidi za uwajibikaji wa kifedha ili kuhakikisha mapato ya kodi yanatumika kwa ufanisi.
Kupitisha hatua zinazofanana zikiwamo za ufuatiliaji wa matumizi kwa wakati halisi na maboresho katika usimamizi wa fedha za umma kunaweza kuimarisha imani ya umma katika sera za kodi huku mapato yakielekezwa kwenye sekta za kipaumbele kama vile afya, elimu na miundombinu.
Kwa Tanzania, taratibu za utekelezaji kama ilivyo katika Kifungu cha 22, zimepitwa na wakati na zinakabiliwa na rushwa na hivyo, kufanya ukwepaji kodi kuwa rahisi. Kutegemea ukaguzi na mbinu duni za ufuatiliaji kumeacha pengo katika ukusanyaji wa mapato.
Korea Kusini ni miongoni mwa nchi zilizotekeleza kwa ufanisi ufuatiliaji wa kodi kidijiti, kutumia Akili Mnemba
kubaini ulaghai pamoja na kutathmini kielektroni viashiria vya hatari ili kuziba mianya hii. Kimsingi, Tanzania inaweza kunufaika na mfumo wa utekelezaji unaoendeshwa na teknolojia, kupunguza utegemezi wa busara za binadamu na kuhakikisha sheria za kodi zinatumika kwa usawa katika sekta zote.
Kwa kuhitimisha mjadala katika mfululizo wa Makala haya dhamira kuu inayobaki wazi ni kuwa, maboresho ya kodi nchini Tanzania lazima yafanyike kwa kina, yawe ya kimkakati na yachukuliwe kwa awamu ili kufikia utulivu wa fedha wa muda mrefu.
Hatua ya kwanza inapaswa kuhusisha matumizi ya mifumo ya kidijiti, ujumuishaji wa mashirika au taasisi za
kukusanya kodi na mipango ya elimu kwa walipa kodi ili kupunguza mizigo ya ulipaji kodi kuongeza ufanisi. Kuhusu muda wa kati, ni muhimu kurahisisha sera za kodi, kuimarisha ufuatiliaji wa matumizi ya umma na kufanya
mikataba ya kuepusha ulipaji kodi maradufu kuwa ya kisasa ili kuimarisha utawala wa fedha.
Maboresho ya kitaasisi ya muda mrefu yanapaswa kujikita katika mifumo ya kisheria kutekeleza nidhamu ya fedha,
uendelevu wa pensheni na mseto wa kiuchumi kwa kuhakikisha vyanzo vya mapato vinazidi kuimarika huku
utegemezi wa ufadhili wa nje ukipungua.
Endapo Tanzania itafuata mbinu hii ya uwazi inayoongozwa na teknolojia, inaweza kujenga mfumo wa kodi wa haki wenye ufanisi na unaozingatia ukuaji unaochochea maendeleo endelevu. Ufanisi katika maboresho hayo utategemea utashi wa kisiasa, ushirikiano endelevu wa wadau kuoanisha sera za kodi na vipaumbele vya kitaifa.
Tanzania inapopitia changamoto zijazo, mafunzo yanayotokana na mfululizo huu yanaweza kutumika kama mwongozo wa kuunda mfumo thabiti wa kodi ambao si tu kwamba unalinda mapato, bali pia unajenga uaminifu,
unahimiza utekelezaji wa sheria za kodi na unafungua njia ya muda mrefu ya ustawi wa kiuchumi.
Shukrani
Kimsingi, uchambuzi huu kuhusu maboresho ya kodi ya Tanzania umefikia hatua nzuri kutokana na michango bora ya wataalamu, watunga sera na wadau mbalimbali.
Hawa ni pamoja na wataalamu wa kodi na wachumi kutoka Tanzania Bara na Zanzibar na hata wachangiaji wa kimataifa kutoka nchi mbalimbali zikiwamo Uingereza, Algeria, Uganda, Kenya, Rwanda, Sudan, Scotland na hata taasisi za kimataifa kama IMF, Benki ya Dunia na mabaraza mengine ya usimamizi wa kodi ambayo pia yamekuwa muhimu katika kuunda ripoti.
Mchango mwingine wa thamani umetoka kwa wawakilishi wa wafanyabiashara nchini, wajasiriamali na wamiliki wa biashara ndogo na za kati katika mikoa mbalimbali ya Tanzania na kwingineko. Kimsingi, uzoefu wao umetoa mwanga kuhusu changamoto za ulipaji kodi.



