Muliro aonya wahalifu sherehe za Pasaka

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limekemea tabia ya watakaojihusisha na vitendo vya uhalifu wakati wa maandalizi ya sikukuu ya Pasaka. Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Jumanne Muliro amesema jeshi hilo linaendelea kusimamia mifumo ya kiusalama ya kuzuia matukio ya uhalifu, kufuatilia na kuwakamata wanaopanga njama na kutenda vitendo ambavyo ni kinyume na sheria za nchi.

“Kumekuwepo na mitazamo kuwa kila inapokaribia wakati wa sikukuu baadhi ya watu hujenga fikra za kujihusisha na vitendo vya kiuhalifu kwa kisingizio kuwa lazima hali hiyo itokee,” alisema Kamanda Muliro alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake na kuongeza:

“Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam halikubaliani na hali hiyo, ulinzi na ufuatiliaji wa mambo mbalimbali upo katika kiwango cha juu na yeyote atakayejihusisha na vitendo vya kihalifu atakuwa katika msuguano mkali na mifumo ya kisheria na atakamatwa atahojiwa kwa kina na baadaye atafikishwa kwenye vyombo vingine vya kisheria,” alisema.

Aliwashukuru wananchi wanaotoa ushirikiano katika kuwabaini wahalifu mapema ili waweze kushughulikiwa. Pia Kamanda huyo wa polisi amewakumbusha wazazi na walezi kuwa karibu na watoto katika kipindi hiki cha sikukuu kuepusha hatari zozote zinazoweza kuwapata.

“Watoto wengi wanapenda kuchezea maji, tunatoa wito kwa wazazi ama walezi kuwa nao karibu wasiachwe wakatembea wenyewe. “Tusingependa kuona watoto wakipotea siku za sikukuu. Tunasisitiza tusiache watoto wenyewe. Wazazi na walezi tuwe na watoto karibu,” alisema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button