Muungano wa Netanyahu watetereka

JERUSALEM : WAZIRI Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amepoteza mshirika mwingine muhimu katika serikali yake ya muungano, baada ya chama cha Kiorthodoksi cha Shas kutangaza kujiondoa serikalini.

Chama hicho chenye misimamo mikali ya kidini, kimetangaza kuwa kinajiondoa kutoka katika nafasi zote serikalini, lakini kimesisitiza kuwa hakitajiunga na upande wa upinzani.

Hatua hiyo imekuja wakati taifa hilo likikumbwa na mvutano mkubwa kuhusu suala la ulazima wa wanaume wa jamii ya Kiyahudi wa dhehebu la Kiorthodoksi kuhudumu jeshini, suala linalopingwa vikali na jumuiya hiyo ya kidini.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya nchini humo, kujiondoa kwa Shas ni pigo kubwa kwa serikali ya Netanyahu, ambayo sasa inaelezwa kupoteza wingi wake bungeni.

Kiongozi wa upinzani, Yair Lapid, amenukuliwa akisema kuwa: Israel sasa inaongozwa na serikali ya wachache baada ya kuondoka kwa chama cha Shas.”

Hali hiyo imezidi kuipa changamoto serikali ya Netanyahu, hasa ikizingatiwa kuwa awali chama kingine cha kidini cha United Torah Judaism kilijitenga na serikali kutokana na mvutano huo huo kuhusu huduma ya kijeshi kwa watu wa imani ya Kiorthodoksi.

Kwa sasa, hali ya kisiasa nchini Israel inaonekana kuyumba, huku wadadisi wa masuala ya siasa wakitabiri uwezekano wa uchaguzi mpya iwapo mvutano hautapatiwa suluhisho la haraka. SOMA: Israel yaendeleza mashambulizi

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button