Mvua yawatenga wananchi wa Kata ya Maboga na wengine

Mvua yawatenga wananchi wa Kata ya Maboga na wengine

WANANCHI wa Kata ya Maboga wilayani Iringa wanakabiliwa na adha ya ukosefu wa huduma ya usafiri wa abiria baada ya barabara yao inayowaunganisha na Kata ya Wasa na Kalenga kuharibiwa kwa kiwango cha kutopitika na mvua zinazoendelea kunyesha.

Pamoja na mvua hizo, mkandarasi aliyepewa zabuni ya kuitengeneza barabara hiyo ya urefu wa kilometa 24, Boimanda Modern Construction Ltd alisitisha kuendelea na ujenzi wake jambo linalozidisha athari kwa wananchi wanaoitegemea kwa shughuli zao mbalimbali za kijamii na maendeleo.

Barabara hiyo inayosimamiwa na Wakala ya Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Wilaya ya Iringa ilianza kutengenezwa kwa vipande vipande na mkandarasi huyo, Oktoba mwaka jana kabla ya ujenzi wake unaotakiwa kukamilika ifikapo mwezi Mei, mwaka huu kusimama Januari, mwaka huu.

Advertisement

Mmoja wa wananchi wa Kijiji cha Makongati katika kata hiyo ya Maboga, Emmanuel Sanga alisema wanalazimika kukodi pikipiki kwa gharama kubwa kwa ajili ya kufuata huduma na bidhaa mbalimbali nje ya kata hiyo.

“Lakini shida kubwa ni pale wananchi wanapotaka kupeleka bidhaa zao za kilimo kama mahindi mabichi sokoni mjini Iringa kwa ajili ya kuuza. Hakuna gari kubwa linaweza kuja kwa sasa katika kata yetu, hii kwa sababu ya kadhia hii ya barabara,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Kiponzero, Allen Dallu alisema ubovu wa barabara hasa katika kipindi cha mvua ni changamoto inayoisibu kata hiyo kwa miaka yote na akawaomba Tarura waangalie uwezekano wa kujenga kwa kiwango cha lami au zege hasa katika maeneo korofi zaidi.

Diwani wa kata hiyo, Veni Muyinga ameishushia lawama Tarura akisema inafahamu changamoto ya barabara hiyo lakini haitaki kuchukua hatua za kudumu ili kuwaondolea taharuki wananchi kila msimu wa mvua unapokaribia au kuanza.

Sekretarieti ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Iringa Vijijini ikiongozwa na Katibu wa Chama hicho, Gama Juma Gama imemnyooshea kidole mkandarasi huyo ikisema hatua yake ya kuondoka katika eneo la mradi bila kutoa taarifa ni dharau kwa wananchi na serikali iliyotoa kodi zao ili kuimarisha barabara hiyo.

“Tunawaomba Tarura wafanye uchunguzi kubaini sababu ya kukwama kwa ujenzi ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa kuwanusuru wananchi wetu na kadhia wanayopata,” alisema Gama.

Mwakilishi wa Meneja wa Tarura Wilaya ya Iringa, Adelick Theonest akijibu malalamiko hayo alisema mvua zinazoendelea kunyesha ndizo ambazo zimesababisha ujenzi wa barabara hiyo usitishwe.

Alisema serikali imetenga zaidi ya Sh milioni 400 kwa ajili ya ukarabati wa barabara hiyo unaotarajiwa kuendelea wakati wowote kuanzia sasa.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *