KIONGOZI wa kanisa la Inuka Uangaze, Boniface Mwamposa amesema agizo la Rais Samia Suluhu Hassan kwa kila mwananchi azingatie mila na desturi za Mtanzania ni silaha ya kupambana na mmomonyoko wa maadili.
Mwamposa amesema hayo alipoongoza ibada ya Jumapili, kwenye madhabahu ya Inuka na Uangaze kwenye makao makuu yake Kawe Dar es Salaam, jana.
“Mawaziri wamezuia matumizi ya vitabu vyenye maudhui yanayohamasisha vitendo vibaya na Rais ambaye ni mama yetu amesema kila mtu azingatie mila na desturi zetu, hili ni jambo la kushukuru Mungu,” alisema.
Mwamposa alisema kushamiri kwa vitendo vya ukiukwaji wa maadili kumefikia kiwango kinachohitaji nguvu za pamoja za viongozi wa kiserikali, kisiasa na kiimani.
Alihimiza viongozi wa kiimani watumie mamlaka hayo kukomesha uovu kwenye jamii.