Mwanasheria Mkuu alivyojipanga utekelezaji Dira 2050

KATIKA Dibaji yake kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 – Dira 2050, Rais Samia Suluhu Hassan anasema Dira 2050 ni mpango thabiti, jumuishi na wenye maono ya mbali, unaoakisi matarajio ya pamoja ya Watanzania na mwelekeo wa kimkakati kwa kipindi cha miaka 25 ijayo.

Anasema Dira 2050 inaweka bayana azma ya kuifikisha Tanzania kwenye ngazi ya juu ya maendeleo, yaani nchi yenye uchumi wa kipato cha kati cha ngazi ya juu utakaoongozwa na maarifa na maendeleo ya viwanda.

Anaongeza kuwa matarajio ni kwamba ifikapo mwaka 2050, Pato la Taifa litakuwa la thamani ya Dola za Marekani trilioni moja na wastani wa pato la mtu mmoja litakuwa Dola za Marekani 7,000 kwa mwaka.

“Ni muhimu kutambua kuwa, Dira 2050 si mpango wa serikali pekee, bali ni mpango wa kitaifa unaotokana na maoni na matarajio ya wananchi na wadau mbalimbali wa maendeleo. Kwa msingi huo, Dira 2050 inaakisi matarajio ya pamoja kuhusu mustakabali wetu na namna ya kuyafikia matarajio,” anaandika Rais Samia.

Anaongeza: “Ili kutimiza malengo ya Dira 2050, ni lazima tujenge utamaduni wa utekelezaji na uwajibikaji wa
pamoja na kuzingatia weledi na ubunifu katika utendaji wetu.” “Hivyo, nitoe rai kwa wizara zote, taasisi za umma,
sekta binafsi, asasi za kiraia, wadau wa maendeleo, vyama vya ushirika na makundi ya kijamii kuhakikisha kuwa
sera, mipango na mikakati ya kisekta zinafungamanishwa na malengo ya Dira hii,” anasema.

Akizindua Dira 2050 kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma, Julai 17, mwaka huu Rais Samia anasisitiza umuhimu wa serikali kutilia mkazo utekelezaji wake kwa kuimarisha mfumo wa uwajibikaji na upimaji wa matokeo ya kazi katika taasisi zote za umma.

Anasema utekelezaji wa Dira 2050 hautakuwa na maana endapo hautafuatiliwa kwa uwazi, umakini na ufanisi. Rais anaielekeza Tume ya Taifa ya Mipango kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu kuandaa haraka mfumo wa kitaasisi wa ufuatiliaji na tathmini utakaoweka wazi majukumu, muda wa utekelezaji na njia za kupima mafanikio katika kila hatua ya utekelezaji.

“Kila taasisi ya Serikali italazimika kuwa na vigezo vya kupima utendaji vinavyoendana na malengo na shabaha ya Dira,” anasema katika uzinduzi huo. “Tutapima kwa matokeo, si kwa maelezo. Ni lazima kila hatua tuone faida yake kwa wananchi,” anasisitiza.

Aidha, naiagiza Tume ya Kurekebisha Sheria na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuanza mchakato wa mapitio ya sheria ili kuziwezesha taasisi mbalimbali kutekeleza dira hiyo kwa ufanisi. Anasema sera zote zisizolingana na mwelekeo wa Dira 2050, lazima zipitiwe na kufanyiwa marekebisho haraka.

Kwa kaulimbiu ya Dira 2050 ya “Tanzania Tuitakayo”, Rais Samia anasema sasa ni wakati wa kuondokana na mazoea na kuingia katika awamu mpya ya kupanga na kutekeleza maendeleo kwa weledi. “Things cannot be business as usual (Mambo yasifanywe kwa mazoea). Lazima tubadilishe namna tunavyofanya kazi,” anasisitiza Rais Samia.

Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Hamza Johari, imejiweka sawa kutelekeza malengo na shabaha za Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ambayo utekelezaji wake unaanza rasmi Julai Mosi, 2026.

Katika mazungumzo maalumu na gazeti la HabariLEO, ofisini kwake jijini Dodoma Machi 10, mwaka huu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Johari ni kama alikuwa mbele ya yale yatakayojiri kutokana na kuwapo kwa Dira 2050.

Johari anafafanua kwa kina namna ofisi yake ilivyojipanga na itakavyosimamia utekelezaji wa dira hiyo kwa upande wa majukumu ya ofisi yake ambayo jukumu kubwa ni kuishauri serikali katika masuala yote ya kisheria ndani na nje ya nchi katika maeneo ya uandishi wa sheria, urekebu wa sheria, ufasiri sheria pamoja na upekuzi na uchambuzi wa mikataba mbalimbali ya kiuwekezaji.

Jukumu lingine ni kutoa ushauri kwa wizara, idara zinazojitegemea na taasisi za serikali kuhusu mchakato wa utungwaji wa sheria na masuala mengine yahusuyo sheria na kutoa ushauri stahiki wa sheria zilizotungwa na Bunge, sheria ndogo na maazimio mbalimbali pamoja na kuandaa miswada ya sheria kwa ajili ya kuwasilishwa bungeni.

Akizungumzia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 hasa eneo la kisheria, Johari anasema Ofisi ya Mwanasheria
Mkuu wa Serikali imeshiriki kikamilifu katika utekelezaji wa maandalizi ya dira hiyo mpya na hata ile inayomalizika mwakani.

“Na pale itakapokuwa imepitishwa sasa na kuanza kutumika, basi na sisi tunaanza utekelezaji wa kuhakikisha kwamba kule tunakotaka kufika mwaka 2050 tunaweza kufika huko,” anasema.

“Kwa sababu kwenye dira tunazungumza kwamba tunataka kuwa taifa ambalo litakuwa limepunguza umaskini kwa kiasi kikubwa, na kuhakikisha kuwa uchumi wetu unakua na na kufikia ile ngazi ya uchumi wa kati wa juu,” anasema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Anafafanua: “Sasa lengo hilo ni kubwa, lakini tunaweza tu kufanikiwa kulifikia kama tu tutahakikisha kila mdau na kila mshiriki wa maendeleo na uchumi anachukua nafasi yake stahiki na kufanya yale ambayo yanapaswa ili kuhakikisha sisi tunafika huko tunakotarajia kufika mwaka 2050.”

Kwa mujibu wa mwanasheria mkuu huyo wa serikali, kwa kuwa dhamira ni kubwa, hana wasiwasi kuwa nchi itaweza kufika huko, na hivyo ofisi yake imejipanga kuhakikisha yale yote yanayoihusu ili kufika huko 2050,  anayafanya ipasavyo.

“Baada ya kuisoma dira ile kwa kina na kuielewa jambo la kwanza ambalo kama Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali tutatakiwa kufanya, ni kuhakikisha kuwa tunalitekeleza na uhakikisha tunaoanisha vizuri sheria zetu tulizo nazo na kule tunakotaka kwenda,” anaeleza Johari.

Anaongeza: “Kwa sababu kule tunakotaka kwenda ili tuweze kufika ni lazima kuwa na hiyo ‘legal framework’ (mpango wa kisheria) wa kutuwezesha kufika kule. Yaani sheria ni kama daraja, la kutuvusha sisi twende. 2025 upande huu na 2050 upande ule, ni lazima tuwe na hilo daraja”.

Anasema kwa msingi huo, sheria zote lazima zioane. Anasema: “Tusipofanya hivyo tutakuwa tunakwenda
kule 2050, lakini sheria zinavuta nyuma”.

Anaongeza: “Ndio maana tunafanya marekebisho ya sheria, lengo ni hilo, ni ili kunyumbulika na jamii inavyokwenda, unanyumbulika na sekta za kiuchumi zinavyokwenda, unanyumbulika na changamoto mbalimbali zinavyokwenda. Kwa hiyo katika dira hii zimedadavuliwa vizuri na jinsi zitakavyokwenda ili kufika 2050,” anasema Johari.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button