Mwanza na mikakati ya uwanja wa ndege wa Kimataifa

MWANZA:Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Amos Makalla amesema Serikali ina Mkakakati wa kuufanya uwanja wa Ndege wa Mwanza kuwa wa Kimataifa kwa kujenga miundombinu ya Kisasa likiwemo jengo la Abiria ambapo amebainisha kuwa tayari zaidi ya Bilioni 11 zipo kwa ajili ya kuanza kwa ujenzi huo.
Makalla ameyasema hayo leo wakati wa Kikao kazi na watumishi wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza ambapo ameagiza pia Mamlaka ya Uwanja wa Ndege kuandaa michoro ya jengo la Abiria, upanuzi, Hoteli na Shopping Mall ili kuleta unadhifu kwenye huduma.
“Nilikuja hapa nikiwa na siku tatu tu Mwanza na nilielekeza muanze ujenzi mara moja tena kwa bahati mna fedha za kuanzia tena ni Bilioni 11 na kazi ya kwanza mliyotakiwa kuanza nayo ni kusanifu namna bora ya ujenzi wa Jengo ambalo litakua la kimataifa ili kuubadilisha uwanja wetu kuwa wa kimataifa.” ….Amesema
Aidha katika hatua nyingine Makalla amesema Shughuli za mamlaka ya viwanja vya ndege pamoja na jeshi la anga kwenye eneo hilo hazipaswi kuingiliwa na wananchi waliovamia na kwamba serikali ipo kwenye uboreshaji wa uwanja huo kuwa wa kimataifa ndio maana kuna shughuli mbalimbali zinaendelea.
Makalla amefafanua kuwa Serikali inaandaa utaratibu wa kuwaondoa wananchi zaidi ya Elfu Moja (Nyumba 800) wa Mitaa ya Mhonze, Kihili na Bukyanhulu waliovamia eneo la Mamlaka ya Uwanja wa ndege ili kutoa fursa kwa shughuli za Uwanja kufanyika katika hali ya Usalama.
“Kwakua Mwanza tunaanza Safari ya kuubadilisha uwanja wa ndege kuwa Uwanja wa kimataifa, Mamlaka inahitaji eneo lote na kwa ajili ya Usalama pia maana jeshi la anga wanalihitaji eneo hilo pia kwa usalama wa ndege zao, za abiria na kwa usalama wa wananchi wetu pia.”…Amesisitiza
Kwa upande wake Meneja wa Uwanja wa Ndege Mwanza, Mussa Mcholla amebainisha kuwa katika kuweka mazingira bora kwa usafiri wa anga nchini serikali imefanya maboresho ya kimkakati yaliyohusisha urefushaji wa Barabara ya kutua na kuruka ndege, ujenzi wa Jengo jipya la abiria na Miundombinu mingine.
 

Habari Zifananazo

Back to top button