Mwenge watembelea miradi miwili kwa malengo maalumu

MWENGE wa Uhuru umeweka mawe ya msingi katika miradi miwili ya maendeleo na kuzindua mradi mmoja na kutembelea miradi miwili kwa malengo maalumu katika Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma.

Miradi iliyowekwa mawe ya msingi ni ule wa jengo la huduma za dharura la Hospitali ya Wilaya ambao hadi sasa umetekelezwa kwa thamani ya Sh milioni 292.3 kati ya Sh milioni 300 zilizotolewa na serikali kupitia mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Covid -19 na mradi wa kisima cha maji katika Kijiji cha Ijaka Kata ya Sagara wenye thamani ya Sh milioni 104.5.

Pia Mwenge umetembelea mradi wa vijana Twende Pamoja Wasakatonge unaojihusisha na uoshaji wa magari na vyombo vingine vya usafiri kupitia mkopo wa Sh milioni saba kutoka halmashauri, huku Shule Shikizi ya Msingi katika Kijiji cha Ibwaga ikikabidhiwa mabati na kiongozi wa Mbio za Mwenge kitaifa, Sahili Geraruma.

Katika hatua nyingine Mwenge wa Uhuru umezindua kituo cha kurusha matangazo ya redio cha Zabibu FM chenye thamani ya Sh milioni 117 ambapo Kiongozi wa Mbio za Mwenge kitaifa, Geraruma amefikisha ujumbe wa sensa kupitia matangazo ya moja kwa moja kituoni hapo kuashiria kituo hicho kutambulika rasmi.

Aidha, katika ujumbe wa Mwenge uliotolewa katika Kijiji cha Mlali na Kibaigwa, wananchi walihamasishwa kushiriki kikamilifu kwenye shughuli ya sensa kwa kuhesabiwa mara moja, kupinga vitendo vya rushwa wakati huo huo wakichukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU).

Mkesha wa Mwenge wa Uhuru ulifanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Kibaigwa huku ukipambwa na wasanii mbalimbali kutoka ndani na nje ya Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa.

Mwenge wa Uhuru ulikabidhiwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule alfajiri ya Agosti 24, 2022 na hatimaye kukabidhiwa mkoani Morogoro.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button