Mwenge waweka jiwe la msingi Hospitali ya Rufaa Ndanda

MWENGE wa Uhuru umeweka Jiwe la Msingi jengo la huduma ya dharura, wagonjwa wa nje (OPD) pamoja na utawala katika Hospitali ya Rufaa ya Ndanda wilayani Masasi, unaogharimu zaidi ya Sh bilioni 1.

Akisoma taarifa ya mradi huo leo, Katibu wa afya wa Hospitali ya Ndanda, Joseph Saibulu amesema hospitali hiyo ina miaka 95 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1927, ilipandishwa hadhi kuwa ya rufaa ngazi ya Mkoa mwaka 2010.

Amesema kwa sasa hospitali hiyo ina uwezo wa kulaza wagonjwa 300, idadi ya wagonjwa wa OPD kwa mwaka ni 85,935, wagonjwa wa ndani (IPD) ni 7,926 kati yao wagonjwa wanaotumia bima ya afya ni 53,347 na wasiyo na bima 32,588.

Advertisement

Mradi wa jengo hilo umefadhiliwa kwa asilimia 100 na Shirika la kimissionari la Wabenedictini pamoja na wafadhili wengine binafsi.

“Mradi huu unafaida mbalimbali kwa wananchi kama vile kuwezesha wagoonjwa wa dharura kupata huduma za matibabu kwa haraka mara tu wanapofika hospitalini na kuwezesha wataalamu wetu kufanya kazi masaa 24 hasa idara dharura”.amesema Saibulu

Mbunge wa Jimbo la Ndanda wilayani humo, Cecil Mwambe amesema wilaya hiyo ina watu wengi ambao wanapatiwa huduma ya afya hospitalini hapo lakini pia nchi jirani kama vile Msumbiji wanakuja hospitalini hapo kupata huduma hiyo.

Amesema serikali ipo kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kwa urahisi kupitia sekta mbalimbali ikiwemo hiyo ya afya.

Baadhi ya wananchi wa Kata hiyo ya Ndanda akiwemo Jane Hamisi “Naishukuru Serikali kutuboreshea hospitali yetu itaturahisishia sisi wananchi kupata huduma kwa haraka na uhakika zaidi”. Amesema Jane.

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Abdalla Shaib Kaim ameridhia na kuweka jiwe la msingi ujenzi huo kutokana umekidhi vigezo na ubora unaostahili.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *