Mwigizaji mwingine nguli Nigeria afariki dunia

NIGERIA: Abuja. MUIGIZAJI, mtayarishaji na muongozaji wa filamu mkongwe nchini Nigeria Amaechi Muonagor, amefariki dunia baada ya kuugua figo, kisukari na kiharusi kwa muda mrefu.
Amaechi alifariki jana akiwa na umri wa miaka 62.
Ndiye aliyeigiza nafasi ya baba wa Aki (Chinedu Ikedieze) na Paw Paw (Osita Iheme) katika filamu ya vichekesho ya Aki na Paw Paw, katika filamu iliyowahi kuwa gumzo nchi mbalimbali.
Mjomba wa marehemu, Tony Muonagor amesema kabla ya kifo chake, muigizaji huyo aliyewahi kuwika katika filamu zaidi ya 250 ikiwemo, Igodo, Aki na Ukwa, Code of Silence na My Village People, amewahi kuomba umma umchangie fedha ili akapandikize figo nchini India.
Amaechi ana shahada ya uchumi aliyoipata mwaka 1987 katika Chuo Kikuu cha Nigeria Nsukka. Anakadiriwa kuwa na utajiri wa zaidi ya dola milioni moja, kwa mujibu wa Austine Media ya nchini Nigeria, fedha hizo zinatokana na uigizaji, uongozaji na uzalishaji wa filamu alizoshiriki lakini pia fedha nyingine amezipata kupitia biashara zake nyingine binafsi.
Amaechi alizaliwa Idemili Jimbo la Anambra Kusini mashariki mwa Nigeria. Ameacha mke na watoto wanne, mchezo aliokuwa akiupenda ni mpira wa miguu na kriketi.
Kifo chake kinakuja wiki chache tu baada ya Nigeria kumpoteza nyota mwingine wa Nollywood John Okafor, anayejulikana zaidi kama Mr.
Ibu, ambaye pia alihitaji msaada wa matibabu.



