Rais Mwinyi afungua Ofisi ya wakala wa ZIPA China

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amefungua rasmi ofisi ya wakala wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) iliyopo Minhang katika Jiji la Shanghai, China.

Katika hafla hiyo fupi ya ufunguzi rasmi wa ofisi, Rais Dk. Mwinyi, amesema kuwa Zanzibar bado inahitaji wawekezaji katika sekta mbalimbali ili kuimarisha na kukuza uchumi wake.

Advertisement

Amesisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

SOMA: Tangazeni fursa za uchumi Zanzibar

Aidha Rais Dk.Mwinyi ameongeza kuwa Serikali ya Zanzibar imedhamiria kuchochea ukuaji wa sekta ya utalii, kilimo, uvuvi, na viwanda ili kuleta maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi.

Kufunguliwa kwa ofisi hiyo ni hatua muhimu ya kufanikisha malengo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, hususan kuvutia uwekezaji na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara baina ya Zanzibar na mataifa mengine.