Mwinyi aiomba UNESCO kusaidia uchumi wa Buluu Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi amelishauri Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) kuisaidia Zanzibar kuendeleza Uchumi wa Buluu kwani ni sekta muhimu kwa Uchumi na Ustawi wa wananchi wake.
Amesema hayo alipozungumza na Ujumbe wa Shirika hilo ukiongozwa na Mkurugenzi wake Mkuu Audrey Azoulay waliofika Ikulu Zanzibar tarehe leo Machi 5.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi.
Dk Mwinyi ameueleza ujumbe huo kuwa kwa sasa sekta ya Uchumi wa buluu ndio kipaumbele cha Serikali kinachohitaji kupewa msukumo wa ziada wa misaada ya kitaalamu, Teknolojia na fedha ili kuwa endelevu na kuiwezesha nchi kunufaika na rasilimali za kutosha zilizomo baharini.
Amesema Uchumi wa buluu una fursa nyingi zinazoweza kutoa mchango mkubwa wa maendeleo na ukuaji wa Uchumi, fursa za ajira na kuimarisha maisha ya wananchi na kuishauri UNESCO kuwa tayari kushirikiana na Zanzibar kuendeleza sekta hiyo.
Rais huyo wa Zanizbar amesema bado zipo changamoto nyingi katika kuuendeleza Mji Mkongwe ili ubaki katika haiba na urithi wake kutokana na kuwa na idadi kubwa ya nyumba zinazohitaji kufanyiwa ukarabati mkubwa, udhibiti wa uingiaji na utokaji wa magari unaopaswa kubadilika kulingana na mazingira ya sasa ndani ya mji huo bila kuathiri maisha ya wakaazi wake.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO Audrey Azoulay ameihakikishia Zanzibar kuwa Shirika hilo litaendelea kushirikiana nayo katika juhudi za kuleta maendeleo endelevu katika sekta tofauti na ustawi wa watu wake.
Amesisitiza kuwa shirika hilo liko tayari kuchukua juhudi maalum na misaada ya kitaalamu, teknolojia na uzoefu kuimarisha sekta ya Uchumi wa Buluu na kupongeza mafanikio yaliyofikiwa katika sekta ya elimu visiwani Zanzibar.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button