Mwinyi Azindua Miradi ya Maendeleo Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imebuni mfumo mpya wa kupata fedha mbadala ili kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kwa haraka bila kutegemea fedha za serikali kuu.

Akizungumza Ikulu Zanzibar katika hafla ya utiaji saini wa miradi mikubwa mitatu yenye thamani ya zaidi ya dola milioni 150, ikiwemo ujenzi wa Hospitali ya Saratani Binguni, Dk. Mwinyi alisema hatua hiyo inalenga kuharakisha utekelezaji wa miradi muhimu ya kijamii na kiuchumi. “Tumekuja na wazo la kupata fedha mbadala, limekubalika, na fedha zitaanza kuwasili. Tutalipa bila matatizo yoyote,” alisema Rais Mwinyi.

Alifafanua kuwa awali miradi mingi ilikuwa ikichelewa kutokana na ukosefu wa fedha, lakini sasa serikali imeweka mpango wa akiba wa dola milioni 15 kwa mwezi kwa ajili ya ulipaji wa madeni, ambapo kwa sasa akaunti hiyo imefikia dola milioni 350. Rais Mwinyi alisisitiza kuwa serikali itaendelea kutumia utaratibu huo ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati.

Miradi iliyosainiwa ni pamoja na mradi wa mpango mkuu wa matumizi ya ardhi na usajili wa hatimiliki, mradi wa maji safi Mkoa wa Kusini Unguja na ujenzi wa Taasisi ya Saratani Zanzibar. SOMA: Mwinyi ataja sekta 11 kipaumbele awamu ijayo

Mradi wa maji utagharimu uro milioni 56 na unatekelezwa na kampuni kutoka India kupitia ufadhili wa benki ya Ujerumani kwa ushirikiano na CRDB Bank. Utahusisha visima 16, matangi 17 na mtandao wa mabomba wa zaidi ya kilomita 150 utakaonufaisha shehia 34.

Aidha, mradi wa ardhi utagharimu uro milioni 43 na unatekelezwa na kampuni ya IGNFI kutoka Ufaransa kwa ufadhili wa BPI France kupitia CRDB, ukilenga kuanzisha mfumo jumuishi wa taarifa za ardhi na vituo vitano vya huduma za ardhi katika mikoa yote.

Kuhusu Hospitali ya Saratani Binguni, alisema itagharimu dola milioni 32.8 na itatekelezwa kwa ubia na kampuni ya Aegle Onco Care Centre Ltd ya Mauritius. “Hizi changamoto za maji, ardhi na tiba ya saratani ndizo zilikuwa kwenye mawazo yangu. Nashukuru tumepata fedha na sasa tunaanza kazi,” alisema Rais Mwinyi. Dk. Mwinyi alizishukuru wizara na mabenki washirika kwa kushirikiana na serikali katika safari ya maendeleo ya Zanzibar, huku akizitaka taasisi za umma kuondoa urasimu ili miradi ikamilike kwa wakati.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button