Mwinyi: SMZ imevuka lengo la Ilani ujenzi wa barabara

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali imevuka lengo la Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) ya 2020-2025 iliyoainisha ujenzi wa kilomita 275 za barabara.
Ameeleza kuwa Serikali imeamua kuongeza idadi ya barabara zitakazojengwa kwa kiwango cha lami hadi kufikia kilomita 300 mijini na vijijini.
Rais Dk Mwinyi ameyasema hayo alipoifungua Barabara ya Ukutini -Bandarini Wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba leo Januari 10.
Aidha, amesema Mkataba wa Wananchi na Serikali yao ni Ilani ya Uchaguzi hivyo kuna kila sababu ya kujivunia kwa yote yaliyofanyika katika ujenzi wa barabara.
Akizungumzia barabara ya Ukutini -Mtangani-Bandarini aliyoifungua amesema ni hatua muhimu ya kufungua fursa za kiuchumi.
Ameeleza kuwa mbali na usafiri barabara hiyo ya Ukutini – Bandarini itafungua fursa za ajira kwa kuwa kuna Bandari na Hoteli katika eneo hilo pamoja kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijami ikiwemo Hospitali, Skuli na Usafirishaji.
Ufunguzi wa Barabara hiyo unakamilisha idadi ya kilomita 85.5 za barabara zilizojengwa katika Mkoa wa Kusini Pemba.
Barabara ya Ukutani – Bandarini yenye kilomita 4.6 iliyojengwa na Kampuni ya IRIS na kugharimu Dola Millioni 2.658 ni miongoni mwa miradi ya ujenzi wa barabara za ndani zenye urefu wa kilomita 275 .9.