Mwinyi: SMZ mstari wa mbele fursa kiuchumi kwa wanawake
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanawake wanapata fursa sawa za kiuchumi kupitia sera na mipango mbalimbali ya uwezeshaji.
Rais Dk Mwinyi amesema hayo alipozungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika Viwanja vya Maonesho Dimani, Mkoa wa Mjini Magharibi leo Machi 6.

Aidha amewahimiza wanawake kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi za uongozi muda utakapowadia.
Dk Mwinyi amefahamisha kuwa kupitia Wakala wa Uwezeshaji Wananchi kiuchumi (ZEEA) wanufaika 34,746 wamefikiwa kati yao hao, 17,811 ni wanawake waliochangia asilimia 51.2 ya wanufaika wote.
Amebainisha kuwa Serikali kupitia Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi imewezesha utoaji wa mikopo yenye thamani ya Shilingi Bilionii 34.9 ambapo Shilingi Bilioni 21 sawa na asilimia 60 zimeelekezwa kwa wanawake.

Kwa upande mwingine, Rais Mwinyi ametoa agizo kwa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Wizara inayoratibu masuala ya majukwaa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda na wadau wote kuandaa utaratibu wa kuhuisha majukwaa ya uwezeshaji wa wanawake kiuchumi ili yalete matokeo yaliyotarajiwa.
Wakati huo huo Rais Dk Mwinyi amezindua Mpango wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto wa 2025-2030 pamoja na Muongozo wa Uanzishwaji wa Majukwaa na Uendeshaji wa Majukwaa ya Wanawake.



