Mwinyi: Zanzibar imepiga hatua haki za wanawake

ZANZIBAR: RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi, amesema Zanzibar imepiga hatua katika kulinda haki za wanawake kwa kuweka sera na sheria bora zinazohakikisha usalama, usawa wa kijinsia na kuwepo kwa miji na maeneo salama ya kijamii.
Rais Dk Mwinyi ameyasema hayo alipoufungua Mkutano wa Saba wa Dunia wa Miji na Maeneo Salama ya Kijamii na Usalama kwa Wanawake unaofanyika katika Hoteli ya Madinat Al Bahr, Mkoa wa Mjini Magharibi leo Agosti 26, 2025.

Ameeleza kuwa kufanyika kwa mkutano huo ni ishara ya Jumuiya ya Kimataifa kutambua juhudi za Zanzibar katika kuwalinda wanawake na wasichana kupitia utekelezaji mzuri wa sera na sheria zinazowahakikishia fursa na ustawi wao.
SOMA ZAIDI
Amefahamisha kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka kipaumbele suala la usawa wa kijinsia kwa kuandaa miji na maeneo salama ya kijamii yanayotoa fursa kwa wanawake kufanya shughuli zao za kijamii na kiuchumi bila hofu, unyanyasaji wa kijinsia na kwa kushirikishwa katika nyanja mbalimbali.

Rais Dk Mwinyi amewahakikishia wananchi, wadau na washirika wa maendeleo kuwa Zanzibar ni nchi salama na wananchi wake wanaendelea kutekeleza shughuli za kimaisha kwa amani na utulivu.
Aidha, ameeleza kuridhishwa na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na taasisi zenye dhamana ya kuwalinda wanawake na wasichana nchini.

Rais Dk Mwinyi amesema Zanzibar imeamua kuwawezesha wanawake kwa kuwaandalia mazingira salama katika maeneo wanayofanyia shughuli zao wakati wote.
Halikadhalika Rais Dk Mwinyi ameishukuru Taasisi ya UN Women kwa mikakati na juhudi zake katika kuhakikisha wanawake duniani kote wanalindwa dhidi ya vitendo vya unyanyasaji.

Kwa upande mwingine, Rais DkMwinyi ametoa wito kwa wadau, taasisi za kikanda na za kimataifa kuungana kwa lengo la kuendeleza miji na maeneo salama na rafiki kwa maendeleo ya wanawake.



