Mzee Kimmich afariki dunia

UJERUMANI: KIUNGO wa Bayern Munich na nahodha wa timu ya taifa ya Ujerumani, Joshua Kimmich, amefiwa na baba yake mzazi, Berthold Kimmich, aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 57, vyanzo mbalimbali vya habari nchini Ujerumani vinaeleza
Taarifa za vyombo vya habari vya Ujerumani zilizochapishwa leo, Oktoba 21, 2026, zimeripoti kuwa kifo hicho kimetokea ghafla, huku klabu ya Bayern Munich ikithibitisha kuwa mchezaji huyo hatakuwa sehemu ya kikosi kitakachoikabili Arsenal katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Klabu hiyo imetoa salamu za pole kwa Kimmich na familia yake, huku ikiomba umma na vyombo vya habari kuheshimu faragha yao katika kipindi hiki cha maombolezo. Bayern ilisema inaungana na mchezaji huyo katika wakati huu mgumu, bila kutoa maelezo zaidi kuhusu mazingira ya kifo hicho.
Kukosekana kwa Kimmich ni pigo kwa Bayern kuelekea mchezo huo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa, kutokana na nafasi yake muhimu katika safu ya kiungo. Hata hivyo, kwa sasa jambo la msingi ni kumpa mchezaji huyo na familia yake nafasi ya kuomboleza msiba huo.



