Nabi ataka makali Nabi ataka makali zaidi Yanga

USHINDI wa mabao 4-1 dhidi ya Singida Big Stars umemfurahisha Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi lakini akasisitiza kuwa bado hawajafi kia kwenye kiwango na ubora wanachokihitaji ndani ya kikosi hicho.

Yanga iliibuka na ushindi huo juzi kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam na kurejea kileleni kwa pointi 26 sawa na Azam inayoshika nafasi ya pili, lakini Yanga ikiwa juu kwa uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Nabi alifafanua kuwa ingawa walipata muda mfupi wa maandalizi, lakini anafurahi kuona wachezaji wake walitambua umuhimu wa mchezo huo, wakafanya kile alichowaelekeza na kubaki kwenye njia salama ya kutetea ubingwa wao.

Pia, alieleza japokuwa wameibuka na ushindi huo, lakini bado wana sehemu nyingi za kurekebisha makosa ili kufikia malengo ya ubora wanaoutaka ndani ya kikosi hicho kulingana na mechi ngumu na michuano mikubwa inayowakabili msimu huu.

“Japo tumepata ushindi huo haimaanishi kwamba muda wote tulicheza vizuri zaidi, vipo vingi vya kusahihisha, kwa namna tunacheza Kombe la Shirikisho Afrika mechi zinazidi kuwa ngumu kwa hiyo lazima kuna makosa turekebishe ili timu ifike tunapopataka.

“Bado hatujafika kwenye malengo tunayoyataka kwamba timu ni bora lakini bado tunaendelea kujitahidi kuhakikisha timu inakuwa bora zaidi ya hapa kwa ajili ya michuano na mechi ngumu zilizo mbele yetu bado,” alisema Nabi.

Kocha wa Singida, Hans Pluijm naye aliipongeza Yanga kwa uwezo mzuri waliouonesha lakini pia ulichangiwa na kikosi chake kutokuwa na mbinu bora, nidhamu na kuwapa nafasi wapinzani wao kuutawala mchezo.

“Nafikiri niipongeze Yanga kwa sababu walitumia nafasi ya kucheza na tukawa tofauti kimchezo kuanzia mbinu, nidhamu na tukapambana kusawazisha mambo uwanjani lakini haikusaidia kitu, nadhani ilikuwa siku mbaya sana kwetu.

“Simba na Yanga ndizo timu kubwa, tunahitaji kupambana na kuwapa changamoto lakini kwenye mechi hii haikuwa vile tulivyopanga. Hakukuwa na ushirikiano kwa mabeki, viungo na washambuliaji, kulikuwa na nafasi kubwa kati yao, hicho ndicho kilichoipa nafasi na muda Yanga wa kuumiliki mchezo na hilo ndilo lilikuwa tatizo letu,” alisema Pluijm.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x