Nabii Mkuu Dk Geo Davie achangia mil 50/-, kampeni za Dk Samia Arusha

KIONGOZI wa Kanisa la Ngurumo ya Upako lenye Makao Makuu yake mkoani Arusha Nabii Mkuu Dk Geo Davie amekabidhi shilingi Milioni 50 kwa Chama Cha Mapinduzi mkoa huo, kuwezesha kampeni za Mgombea Urais wa CCM Dk Samia Suluhu Hassan anayetarajiwa kuwa na mikutano yake ya kampeni mwanzoni mwa mwezi ujao.
SOMA: ‘Viongozi wa dini unganisheni Watanzania’
Akikabidhi fedha hizo leo Septemba 25, 2025 kwenye Makao Makuu ya Chama hicho Mkoa wa Arusha, Nabii Geo Davie amemueleza Katibu Mkuu wa CCM Mkoa, Musa Matoroka kuwa anajisikia fahari kuchangia chama chake, akimtakia kheri Dk Samia kwenye kampeni zake.

“Nashukuru kwa fursa ya kuchangia Chama chetu, Chama Cha Mapinduzi CCM hasa katika ujio tunaoutarajia Mkoani Arusha wa Mwenyekiti wa Chama Taifa na hasa wakati huu wa kuelekea uchaguzi Mkuu,” amesema Dk Geo Davie.

Kwa upande wake Matoroka kwa niaba ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha amemshukuru Nabii Mkuu Geo Davie kwa mchango wake huo wa hiari, akimueleza kuwa Chama Cha Mapinduzi na serikali wanaunga mkono jitihada zake katika malezi ya kiroho kwa waumini wake pamoja na usaidizi wake katika shughuli za maendeleo kwenye Mkoa wa Arusha.



