Nape mgeni rasmi mkutano wa kitaaluma TEF

WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape, Nnauye anatarajia kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa mkutano wa 12 wa kitaaluma wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), utakaonyika kuanzia Machi 29 hadi 31, mwaka huu mkoani Morogoro.

Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa Jukwaa hilo , Neville Meena amesema hayo kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leoMachi 27,2023  mjini Morogoro.

Meena amesema  kila mwaka jukwaa linakuwa na mkutano wa kitaaluma  na wahariri wanakutana na kujadiliana masuala mbalimbali ya kitaaluma na kwa mwaka huu utafanyika mkoani Morogoro.

“ Katika mkutano huu tumemuomba waziri wetu Nape kuwa mgeni rasmi wa kutufungulia mkutano wetu na mpaka sasa amethibitisha kuwa atakuwa na sisi,” amesema Meena.

Amesema katika mkutano huo mambo yatakayojadiliwa ni pamoja na mawasilisho ya ndani ya TEF, yenye mada sita ikiwemo ya utendaji wa  vyombo vya habari kitaaluma na maadili.

“ Tukiwa wahariri tuna jukumu la kusimamia maadili katika vyumba vyetu vya  habari, kwani maadili yanatuhusu tukiwa waandishi wa habari,“ amesema Meena.

Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa Jukwaa hilo, Jane Mihanji ametaja mada nyingine ni wanawake katika habari na hatari ya kutoweka kwao ndani vyumba vya habari.

Mada nyingine ni masuala ya uchaguzi na nafasi ya vyombo vya habari kuanzia kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2024 pamoja na uchaguzi mkuu wa 2025.

Alitaja mada nyingine ni kuhusu uchumi ndani ya  vyombo vya habari na kujinusuru  na namna ya kukabiliana nayo.

Nyingine ni mabadiliko ya teknolojia, ukuaji na ujenzi wa mitandao ya kijamii yenye viwango vya kitaaluma.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button