Nape: Oktoba 29 nendeni mkamalize kazi!

TANGA: MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mgombea Ubunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye, amesema kuwa CCM haikufanya makosa kumteua Dk. Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wa urais kwa mara nyingine, kwani tayari ameonesha kwa vitendo uwezo na ufanisi wake katika uongozi.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni za urais wa CCM uliofanyika mkoani Tanga, Nape amesema utekelezaji wa majukumu ya Dk. Samia katika kipindi chake cha uongozi umekuwa wa mfano na umesaidia kurahisisha mchakato wa uteuzi wake kuwa mgombea wa urais kwa mara ya pili.
“Mimi ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM. Kabla ya kumteua Dk. Samia kuwa mgombea wa urais, tulipokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi kupitia vikao vya NEC na Halmashauri Kuu. Tuliona kazi kubwa aliyofanya,” amesema Nape.
Amefafanua kuwa Dk. Samia alipopewa jukumu la kusimamia utekelezaji wa Ilani, alipewa kazi ya kuhakikisha umeme unafika katika vijiji vyote nchini. Hata hivyo, alikwenda mbele zaidi na kupeleka umeme hadi kwenye zaidi ya asilimia 54 ya vitongoji, jambo ambalo halikutarajiwa.
“Wapo wanaosema ukiona vyaelea ujue vimeundwa. Sasa aliyeviunda ndiye huyu tunayemleta mbele yenu,” amesisitiza.
Nape aliwataka Watanzania kujitokeza kwa wingi Oktoba 29 na kwenda kulipa deni kwa kumpigia kura za kutosha Dk. Samia Suluhu Hassan, ili aendelee na kazi nzuri aliyoianza.
Aidha, ameeleza kuwa Dk. Samia alipoingia madarakani alielekeza nguvu katika sekta zenye mchango mkubwa katika ajira, kama vile kilimo. Alisema bajeti ya kilimo imeongezeka kutoka Shilingi bilioni 294 hadi kufikia Shilingi trilioni 1.2, hatua ambayo imewavutia wakulima na kuleta matokeo chanya.
“Sisi ni chama cha wakulima. Bajeti imeongezeka kiasi hicho, kwa nini tusiendelee kumuunga mkono? Wakati washirika wa maendeleo hawakupendelea utoaji wa ruzuku, Dk. Samia aliamua kusimama na wananchi wake. Alisema liwalo na liwe, na leo hii uzalishaji umeongezeka na ruzuku inatolewa,” amesema.
Nape amehitimisha kwa kuwaambia wanachama wa CCM kuwa na fahari na kutembea kifua mbele kwa sababu wanaye mgombea ambaye anatekeleza kwa vitendo Ilani ya chama chao.