NBC yakabidhi Kombe la Vijana (U20) kwa Kagera Sugar FC

DAR ES SALAAM: MDHAMINI Mkuu wa Ligi ya Vijana chini ya miaka 20 (U20 Youth League) Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imekabidhi kombe la ubingwa wa ligi hiyo kwa timu ya Kagera Sugar FC yenye maskani yake mkoani Kagera baada ya timu hiyo kuibuka bingwa wa ligi hiyo kwa msimu wa 2023/2024 kufuatia ushindi wake wa penati 3-2 dhidi ya wenzao Dodoma Jiji FC (U20).

Hafla ya kukabidhi kombe la ubingwa huo ilifanyika jana katika uwanja wa Chamazi Complex jijini Dar es Salaam ikihusisha ushindani mkubwa baina ya timu hizo mbili hali iliyosababisha hadi dakika 90 zinakamilika matokeo yakiwa 0-0 na hata zilipoongezwa dakika nyingine 30 bado matokeo yalibakia kuwa hivyo hivyo na hatimaye mshindi kuamuliwa kwa njia penati.

Mkurugenzi wa Hazina na Masoko ya Fedha wa Benki ya NBC Bw Peter Nalitolela aliiwakilisha benki hiyo kwenye tukio hilo lililopambwa na uwepo wa mashabiki na wadau mbalimbali wa mchezo huo wakiongozwa na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia.

Wachezaji wa Kagera Sugar FC (U20) wakijipongeza baada ya timu hiyo kuwa bingwa wa Ligi ya Vijana (U20) kwa msimu wa 2023/2024. Hafla ya kukabidhi kombe la ubingwa huo ilifanyika jana katika uwanja wa Chamazi Complex jijini Dar es Salaam ambapo ilishuhudiwa mabingwa hao wakishinda kwa mikwaju ya penati 3 -2 dhidi ya wenzao wa Dodoma jijini. Benki ya NBC ni mdhamini mkuu wa ligi hiyo.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Nalitolela alisema tukio hilo limehitimisha utoaji vikombe vya ligi zote tatu zinazodhaminiwa na benki hiyo kwa msimu 2023/2024 ambapo tayari benki hiyo ilianza kwa kukabidhi kikombe cha cha Ligi ya Championship kwa timu ya Kengold ya mkoani Mbeya mapema mwezi huu huku makabidhiano ya kikombe kingine yakiwa ni yale yaliyofanyika mwishoni mwa wiki ambapo ilishuhudiwa benki hiyo ikitumia helkopta kuleta kikombe cha Ligi Kuu ya NBC kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam kabla ya kukabidhi kwa mabingwa wa ligi hiyo timu ya Yanga SC yenye maskani yake mtaa wa Jangwani jijini Dar es Salaam.

“Kimsingi tunawapongeza sana vijana wa Kagera Sugar (U20) kwa mafanikio haya na hivyo wanaungana na mabingwa wengine wawili ambao tayari wamefamikiwa kutwaa vikombe hivi vya NBC kwa msimu wa 2023/2024. Msukumo wa NBC kudhamini ligi hii ya vijana unachagizwa na dhamira yetu ya kuwa na ligi kuu yenye ubora na ushindani kutokana na vipaji vinavyozalishwa hapa nchini.’’

“Umuhimu wa uzalishaji wa vipaji hivi unaonekana pia hata kwenye timu ya taifa. Hivyo huu ni mwanzo tu tutaendelea kuboresha zaidi udhamini wetu ili kupata matunda mazuri zaidi,’’ alisema Nalitolela.


Mkurugenzi wa Hazina na Masoko ya Fedha wa Benki ya NBC, Peter Nalitolela (wa tatu kulia) akiwapongeza wachezaji wa Kagera Sugar FC (U20) baada ya timu hiyo kuwa bingwa wa Ligi ya Vijana (U20) kwa msimu wa 2023/2024. Hafla ya kukabidhi kombe la ubingwa huo ilifanyika jana katika uwanja wa Chamazi Complex jijini Dar es Salaam ambapo ilishuhudiwa mabingwa hao wakishinda kwa mikwaju ya penati 3 -2 dhidi ya wenzao wa Dodoma jijini. Benki ya NBC ni mdhamini mkuu wa ligi hiyo.

Zaidi Nalitolela alibainisha kuwa kukamilika kwa ligi hizi kunatoa fursa kwa benki hiyo kuendeleza programu zake nyingine za michezo ikiwemo kiliniki yake ya vipaji kwa watoto wadogo yaani NBC Football Kliniki sambamba na maandalizi ya mbio za NBC Dodoma Marathon zinazotarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni zikiwa na lengo la kukusanya fedha kwa ajili kusaidia matibabu na upimaji wa saratani ya shingo ya uzazi kwa wananawake sambamba na kufadhili masomo ya wakunga hapa nchini.

Akizungumzia baadhi ya mafanikio ya udhamini wa benki hiyo kwenye ligi hizo, Nalitolela alisema umeambatana na matokeo chanya hata nje mchezo husika ambapo kupitia mnyororo wa sekta ya mchezo benki hiyo imeweza kuzalisha ajira za takribani 7,000 kupitia udhamini huo.

SOMA: Michuano ya vijana Afrika yarindima Unguja

Habari Zifananazo

Back to top button