ZANZIBAR: Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi ametoa wito kwa jamii kuendelea na jitihada zake za kuwawezesha wanawake katika nyanja mbalimbali za maisha, ili kuharakisha kasi ya maendeleo ya taifa.
Katika salaam zake za heri kwa wanawake wote, katika Siku ya Wanawake Duniani, leo Machi 8, Nchimbi, akirejea kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu 2024, amesisitiza umuhimu wa kuwekeza kwa wanawake ili kuharakisha maendeleo na ustawi wa jamii kwa taifa.
“Kama kauli mbiu yetu ya mwaka huu inavyosema Wekeza kwa Wanawake: Kuharakisha Maendeleo ya Taifa na Ustawi wa Jamii, inatuhimiza umuhimu wa kuwawezesha wanawake katika jamii yetu, kiuchumi, kielimu, na kisiasa ili kuchangia kasi ya maendeleo ya Taifa na kuboresha ustawi wa jamii kwa ujumla, “amesema Nchimbi
Amesema, kwa upande wa CCM wanajivunia kuwa mfano mzuri, kwa kuishi na kaulimbiu hiyo kwa kuwa na mifumo imara katika kutambua nafasi za wanawake na vipawa mbalimbali walivyonavyo.
Aidha, Nchimbi ametumia fursa hiyo kuungana na Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuwatakia wanawake wote Heri ya Siku ya Wanawake Duniani, huku akitambua mchango mkubwa wa wanawake katika kujenga ustawi wa jamii nzima na watu wake.
Amesema, CCM kama chama tawala, chenye dhamana ya kutoa uongozi wa nchi, kinajivunia na kutambua mchango wa viongozi mahiri na shupavu ndani ya Jumuiya ya Umoja wa Wanawake (UWT).
“Kipekee, tunajivunia jumuiya yetu ya UWT inayoongozwa na Mary Chatanda. kwa hakika jumuiya hiyo iliyoasisiwa na Hayati Bibi Titi Mohamed kwa kiasi kikubwa imechangia kuandaa viongozi mahiri wa nchi hii,” amesema Nchimbi
Amesema, viongozi kama Bibi Titi Mohamed, Mwanamajumui wa Afrika na Sofia Kawawa ni mojawapo ya matunda ya taasisi hiyo.
Amesema CCM itaendelea kuhakikisha wanawake wanapata fursa sawa katika nyanja zote za maisha, ikiwemo elimu, afya, ajira, uongozi, na maamuzi.