Ndejembi akemea wizi kwa watumishi wa umma

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deo Ndejembi amekemea tabia ya baadhi ya watumishi wa umma nchini kujihusisha na vitendo vya wizi ambavyo vinakwenda kinyume na dhamira ya Dk. Samia Suluhu Hassan ya kuujenga Utumishi wa Umma wenye uadilifu.

Akizungumza na Watumishi wa Umma wa Manispaa ya Wilaya ya Ilala, Ndejembi amesema Dk. Samia ana maono makubwa ya kuujenga utumishi wa umma wenye uadilifu, hivyo amewataka watumishi wa umma nchini kutokumuangusha badala yake wafanye kazi kwa bidii na uadilifu mkubwa katika kulitumikia taifa.

“Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amejipambanua wazi kututhamini watumishi wa umma kwa kuboresha maslahi na stahili zetu hivyo, hatuna budi kufanya kazi kwa bidii na uadilifu ili kuunga mkono kwa vitendo dhamira yake ya kuujenga Utumishi wa Umma wenye uadilifu na unaowajibika kwa wananchi,” Ndejembi amesisitiza.

Aidha, Ndejembi amewataka Watumishi wa Umma kutafakari madhara ya wizi na kutathmini mienendo yao ili kutokuwa ni sehemu ya kukwamisha dhamira ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha huduma kwa wananchi na kuliletea taifa maendeleo katika sekta zote muhimu kama vile afya, kilimo, uvuvi, biashara, uwekezaji na miundombinu.

Ndejembi pia amewataka Waajiri na Maafisa Utumishi Serikalini kuwasimamia vema watumishi wanaowaongoza badala ya kusubiria mpaka viongozi wa juu wa kitaifa kufika katika maeneo yao ya kazi kukemea uovu pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma.

Akizungumzia matumizi ya fedha za umma, Ndejembi amesema kuwa fedha za umma zinapaswa kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa na Serikali kwani kinyume na hilo ni ukosefu wa maadili katika Utumishi wa Umma.

Ndejembi ameeleza bayana kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita haitomvumilia mtumishi yeyote atakayekwenda kinyume na maadili ya Utumishi wa Umma kwa kujihusisha na vitendo vya wizi katika eneo lake la kazi.

Habari Zifananazo

Back to top button