Ndugai kuzikwa kwao J’tatu

SPIKA mstaafu wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai (62) anatarajiwa kuzikwa Jumatatu ijayo kijijini kwake Sejeli katika Kata ya Sejeli wilayani Kongwa Mkoa wa Dodoma.

HabariLEO ilifika nyumbani kwake Njedengwa katika Manispaa ya Dodoma eneo la nyumba za viongozi ambako uko msiba wa mwanasiasa huyo aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kongwa kwa miaka 25 hadi mauti yanamkuta juzi Agosti 6, mwaka huu.

Binamu wa Ndugai, Anderson Sagala alisema familia hiyo inaendelea na mipango ya mazishi ya ndugu yao yatakayofanyika katika Kijiji cha Sejeli.

“Mazishi ya mpendwa wetu yatafanyika Kongwa na ibada ya mazishi itafanyika Jumapili katika Uwanja wa Mpira Kongwa,” alieleza Sagala na kuongeza kuwa kabla ya kumhifadhi katika nyumba ya milele, pia itafanyika ibada nyingine.

Mdogo wa Ndugai, Baraka Joseph alisema alifika nyumbani kwa Ndugai juzi na kupokelewa kwa upendo, alihudumiwa kwa ukaribu na akampa fedha kwa ajili ya mafuta ya pikipiki, baada ya hapo hakuipata simu yake tena.

Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma, Jawadi Mohamed alisema mkoa huo umepoteza nguli wa siasa na hazina kubwa ya maarifa ambaye alitoa mchango mkubwa katika mkoa huo.

“Kifo cha Ndugai kimeacha pengo kubwa katika Mkoa wa Dodoma,” alisema Mohamed.

Katika makazi ya Ndugai, pia viongozi wa siasa, serikali na watu mbalimbali walifika kuwapa pole ndugu na jamaa na kuulizia utaratibu wa maziko.

Waliokuwa wabunge wa Mkoa wa Dodoma ambao Ndugai alikuwa mwenyekiti wao, wamemtaja kwamba alikuwa alama yao na chuo cha kuwafunda wengine.

Aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu ambaye ameshinda kura za maoni Jimbo la Kondoa Mjini, Mariam Ditopile (CCM) alisema kwake hana cha kuzungumza zaidi ya kusema apumzike kwa amani.

“Tumempoteza kiongozi ambaye aliipenda nchi yake kwa dhati na aliipenda sana Dodoma,” alisema Mariam.

Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Dodoma ambaye ameshinda kuwa za maoni katika jimbo jipya la Mtumba, Anthony Mavunde (CCM), alieleza namna Ndugai alivyokuwa na matamanio ya maendeleo kwa Mkoa wa Dodoma.

“Kama Mwenyekiti wetu wa Wabunge wa Mkoa wa Dodoma alitamani kuona maendeleo ya Dodoma yanakua kwa kasi kubwa hasa mkazo wake mkubwa siku zote ulikuwa ni kwenye kuwajengea mfumo mzuri watoto wa Dodoma kupata elimu bora,” alisema Mavunde ambaye pia ni Waziri wa Madini.

Alisema wataendelea kusisitiza juu ya umuhimu wa elimu kwa jamii ya wana-Dodoma kama njia nzuri ya kumuenzi Ndugai.

 

Mbunge wa Mvumi, Livingstone Lusinde (CCM) alisema aliyefariki ni mwalimu wake kwenye siasa, lakini anamkumbuka kwa misimamo yake katika kuamua mambo hasa kunapotokea mkwamo.

 

Lusinde maarufu kwa jina la ‘Kibajaji’ aliongeza kuwa anamkumbuka Ndugai alivyokuwa akimtia moyo mwaka 2005 wakati huo akiwa Katibu Msaidizi wa CCM Wilaya ya Kongwa na kumtabiria mema bila kumkatisha tamaa.

 

Ibada kaburini

Jumanne wiki hii, Ndugai alikwenda kufanya ibada kwenye kaburi la mama yake.

Mdogo wa Ndugai, Bahati Chonya alisema hayo juzi usiku alipozungumza na Kituo cha Televisheni ya Mtandaoni ya Millard Ayo, nyumbani kwa Ndugai maeneo ya Majengo Mapya wilayani Kongwa.

Chonya alisema Jumanne wiki hii, Ndugai baada ya kuamka asubuhi alikuwa anasikiliza kwaya kwa kutumia spika ndogo.

“Akatoka ndani, lakini alituambia kama ana mafua kidogo tutoke nje… bahati nzuri baada ya muda kidogo akaja Mheshimiwa Diwani na Mwenyekiti wa Kata ya Kongwa Mjini na Katibu tukaongea ongea hapo, lakini akawa anataja anataka kwenda kijijini Ibwaga ambako marehemu mama amezikwa hapo,” alieleza Chonya.

Alieleza kuwa kwa kawaida wakati wa uchaguzi kabla au baada, huwa wanafanya ibada kwenye kaburi la mama yao.

Jumanne wiki hii ilikuwa siku moja baada ya kura za maoni za wagombea wa ubunge wa CCM nchini kote ambazo Ndugai aliongoza kwa Jimbo la Kongwa.

“Kwa hiyo ilivyofika muda wa mchana mchana hivi tukapewa chakula tukala, na yeye mwenyewe akala, baada ya kumaliza tukio la kula tukaenda kijijini Ibwaga. Bahati nzuri tukafika pale tukafanya ibada kidogo akaniambia anakwenda Dodoma,” alifafanua Chonya.

Chonya alisema walivyotoka kijijini, Ndugai alipita katika Ofisi ya CCM Wilaya ya Kongwa kumuona katibu na alipotoka hapo aliondoka kwenda Dodoma Mjini.

“Alikuwa na furaha tu kawaida, tukaongea habari za uchaguzi na mambo mengine… hakuwa na shida yoyote, maana hata kwenye gari alipanda mwenyewe mpaka kule kijijini tulivyofika tulipomaliza ibada akawa anataniana na wachungaji pale na akatoa sadaka,” alibainisha mdogo huyo wa Ndugai.

Imeandikwa na Magnus Mahenge (Dodoma) na Eva Sindika (Dar).

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button