Ndumbaro ateta na watumishi wa Wizara

DODOMA:  Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo  Dk. Damas Ndumbaro ameagiza Watumishi wa wizara kuitumikia wizara hiyo kwa kuzingatia falsafa ya kujitambua, kufanya tathmini na kutekeleza kwa ufasaha majukumu yalipangwa katika wizara hiyo kwa maendeleo ya nchi.

Ndumbaro ametoa maagizo hayo wakati akifungua Baraza la Wafanyakazi kwa mwaka 2023/24 ambalo limefanyika  Novemba 16, 2023 Jijini Dodoma na kusisitiza ushirikiano wa utekelezaji wa majukumu kati ya wizara na taasisi zake.

“Hii ni wizara ya furaha, ajira na uchumi, katika kutekeleza hilo, lazima tuwe wa ubunifu kila mmoja katika eneo lake, lazima tufanye kazi kwa bidii, tuimarishe mawasiliano ndani ya wizara, upendo na zaidi sana tuoneshe wizara hii ina mchango gani katika ukuaji wa uchumi pamoja na idadi ya ajira kwa taifa letu” amesema Ndumbaro.

Aidha, Ndumbaro ameongeza kuwa wizara hiyo imeanza safari ya mabadiliko na kuwataka watumishi wote wa Wizara na taasisi kusonga mbele ili wizara iendelee kushika nafasi yake na kuwaahidi watumishi hao safari hiyo itakuwa nzuri sana na yenye mafanikio.

Awali Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Gerson Msigwa amesema wizara hiyo inaendelea na majukumu yake na kubwa zaidi sekta zake za utamaduni, sanaa na michezo zinaendelea kutangaza vyema nchi, pamoja na kuendelea kutengeneza fursa na ajira kwa wadau na jamii kupitia mazingira bora yaliwekwa.

Amewasisitiza wajumbe wa baraza hilo, kuendelea kuwa wawakilishi wazuri wa wenzao na kutoa mrejesho wa baraza, pamoja na kuendelea kufanya kazi kwa bidii, kufuata sheria, miongozo, kanuni na taratibu na utumishi wa umma.

Baraza hilo pamoja na mambo mengine limepokea taarifa ya Bajeti ya Mwaka 2023/24 ambayo imeanza kutekelezwa katika sekta za wizara ikiwemo ujenzi wa viwanja na maeneo ya kupumzikia katika Jijini la Dar es Salaam na Dodoma na kusisitiza kuwa wizara hiyo ni wizara nyeti hivyo watumishi hawana budi kufanya kazi kwa bidii ili kuwaonesha watanzania umuhimu wa wizara hiyo.

Habari Zifananazo

Back to top button