Ndumbaro: Migogoro ardhi inasababishwa na watumishi

WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro amesema kuwa migogoro mingi ya ardhi nchini inasababishwa na baadhi ya watumishi wa umma wasio waaminifu katika Idara ya Ardhi wanaotumia nafasi zao vibaya na kusababisha unyanyasaji kwa wananchi.

Dk Ndumbaro alitoa kauli hiyo jijini Arusha wakati wa kampeni ya Mama Samia Legal Aid katika viwanja vya Kata ya Kaloleni, sambamba na maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, ambayo kitaifa yanafanyika mkoani humo.

Alisema serikali haitasita kuchukua hatua kali kwa watumishi wa umma wanaohusika na dhuluma za ardhi, akiwataka kubadilika kabla ya hatua madhubuti kuchukuliwa dhidi yao.

“Nimekuja kuweka kambi Arusha pamoja na timu ya wanasheria zaidi ya 50 ili kutatua migogoro ya ardhi kwa wananchi. Kila mwenye haki atapata haki yake,” alisema Ndumbaro.

Aliongeza kuwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inalenga kuhakikisha kila mwananchi anapata haki bila upendeleo wala dhuluma.

Dk Ndumbaro alibainisha kuwa licha ya hatua zilizochukuliwa dhidi ya baadhi ya watumishi wa umma waliokiuka  maadili, bado kuna wachache ambao hawajabadilika watakaochukuliwa hatua stahiki.

Akizungumzia unyanyasaji wa kijinsia, alisema kuwa kwa muda mrefu limekuwa likiwakumba zaidi wanawake na watoto lakini hali imeanza kubadilika kwani na wanaume wanakumbwa.

“Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 53 ya watu waliopokea msaada wa kisheria kupitia kampeni ya Mama Samia Legal Aid ni wanaume, huku asilimia 47 wakiwa wanawake. Hali hii inaonesha kuwa unyanyasaji wa kijinsia si tatizo la jinsia moja pekee,” alisema Ndumbaro.

Alifafanua kuwa huduma hiyo ya msaada wa kisheria imeshatolewa katika mikoa 22, huku mikoa tisa iliyobaki ikitarajiwa kufikiwa hivi karibuni.

Alisema miongoni mwa migogoro inayotatuliwa katika mikoa hiyo, mingi ni ya ardhi ambayo wanawake wengi hudhulumiwa katika mirathi.

Kuhusu ndoa za utotoni, Waziri Ndumbaro alisema tatizo hilo bado lipo katika baadhi ya maeneo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button