NECTA imechukua uamuzi sahihi maarifa lugha za kigeni

BARAZA la Mitihani la Tanzania (NECTA) limeandika ukurasa mpya katika historia ya elimu nchini kwa kujumuisha lugha za kigeni katika upimaji wa kitaifa wa darasa la nne.
Masomo yaliyoingizwa ni Kifaransa, Kichina na Kiarabu.
Hatua hii ni ya kupongezwa kwa dhati kwani inaonesha mwelekeo chanya wa serikali katika kuandaa kizazi chenye uwezo mpana wa mawasiliano kimataifa watakaokidhi mahitaji ya dunia ya sasa inayounganishwa na teknolojia, biashara, diplomasia na utamaduni.
Tanzania, kama ilivyo kwa mataifa mengine yanayoendelea, inakabiliana na changamoto ya kuandaa rasilimali watu yenye ushindani wa kimataifa.
Kuanzishwa kwa mitihani ya lugha hizo tatu katika ngazi ya shule za msingi ni hatua ya kimkakati inayowezesha watoto kujenga msingi imara wa ujuzi wa lugha mapema.
Tafiti mbalimbali za kielimu zinaonesha kuwa mtoto anapojifunza lugha zaidi ya moja katika umri mdogo, uwezo wake wa kufikiri, kuelewa na kufanya uamuzi unakuwa mkubwa zaidi.
Hivyo, Necta imechukua uamuzi muafaka unaolenga si tu kukuza maarifa ya lugha, bali pia kukuza fikra za kimataifa miongoni mwa watoto.
Kwa kuanzishwa kwa upimaji huu, serikali kupitia Necta imeonesha dhamira ya dhati ya kufungua milango ya fursa kwa wanafunzi wa Tanzania kushiriki kikamilifu katika ulimwengu wa sasa wa utandawazi.
Tunatambua kwamba Kifaransa ni muhimu katika nchi nyingi za Afrika na taasisi za kimataifa huku Kichina ikiwa ni lugha kuu ya uchumi unaokua kwa kasi duniani.
Vilevile Kiarabu ni lugha ya biashara na hata kijamii hasa katika eneo la kiimani katika maeneo mengi ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini.
Kwa hivyo, wanafunzi wanaopata ujuzi wa lugha hizi tangu wakiwa wadogo watakuwa na nafasi nzuri zaidi katika ajira, elimu ya juu na ushirikiano wa kimataifa katika siku zijazo.
Tunapongeza pia shule 115 za msingi ambazo zimeingia katika hatua hii ya mwanzo na ambazo zimekuwa mfano kwa kuona mbali.
Tunahimiza shule nyingine hususani za serikali kufuata nyayo hizo bila kuachia jukumu hilo la kuendeleza masomo ya lugha za kigeni kuwa la shule binafsi pekee.
Ni matumaini yetu kwamba serikali, kupitia Wizara ya Elimu itahakikisha walimu wenye taaluma ya lugha hizo na nyinginezo wanapatikana na vitabu vya kufundishia vinaboreshwa ili kutoa nafasi sawa kwa shule zote nchini.
Kwa upande mwingine, wazazi na jamii kwa ujumla wanapaswa kuelewa umuhimu wa kuwahimiza watoto wao kujifunza lugha zaidi ya Kiswahili na Kiingereza.
Ujuzi wa lugha nyingi ni nyenzo ya maarifa, diplomasia, biashara na maendeleo binafsi. Tunahimiza hatua hii iwe endelevu kwa maana usajili huu usiwe tukio la kwanza na la mwisho bali iwe mwanzo wa mapinduzi mapya katika elimu ya lugha nchini.
Kwa ujumla, Tanzania inajitengenezea daraja jipya la mawasiliano na dunia kupitia kwa watoto hao wa darasa la nne. Hii ni hatua muhimu na ya kimkakati kwa mustakabali wa taifa.
JOIN US Everybody can earn 250/h Dollar + daily 1K… You can earn from 6000-12700 Dollar a month or even more if you work as a part time job…It’s easy, just follow instructions on this page, read it carefully from start to finish… It’s a flexible job but a good earning opportunity. tab for more detail thank you……..
THIS→→→→ http://www.job40.media