Ngajilo kuvitambua vilabu vya pombe kama chanzo cha uchumi Iringa Mjini

IRINGA:: Mgombea ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini kwa tiketi ya CCM, Fadhili Ngajilo, amesema ni wakati wa kuviheshimu vilabu vya pombe na kuvitambua kama sehemu halali ya uchumi wa wananchi, badala ya kuviangalia kama maeneo ya watu wa chini au wahalifu.

Akizungumza katika kata ya Mwangata, Ngajilo alisema vilabu vya pombe vimekuwa vikitengeneza ajira, kusomesha watoto na kuchangia maendeleo ya familia nyingi za mjini Iringa, hivyo vinapaswa kuwekewa mazingira rafiki ya kibiashara.

“Vilabu vya pombe vihesimishwe, tusivichukulie kama ni maeneo ya watu wa chini. Wapo watu wengi wamesomeshwa kwa biashara hizo hizo. Ni biashara halali, na tutatunga kanuni zitakazowaongezea uhuru wa kufanya biashara bila bughudha,” alisema.

Ngajilo alisisitiza kuwa, akipewa ridhaa na wananchi, atahakikisha wafanyabiashara hao wanapatiwa elimu ya uendeshaji bora wa biashara na mitaji midogo kupitia taasisi mbalimbali za kifedha, ili kuongeza tija katika shughuli zao.

“Tutakaa na wafanyabiashara, tutasikiliza changamoto zao na kuandaa ushauri utakaoboresha biashara zao.
Mtapata pia mafunzo ya ujasiriamali na kilimo cha kisasa ili mpate kipato zaidi,” aliongeza.

Aidha, alisema changamoto ya mitaji ndani ya kata ya Mwangata ni miongoni mwa mambo yatakayopatiwa kipaumbele kupitia ushirikiano na taasisi mbalimbali za kifedha, ili wananchi wa chini waweze kujikimu kiuchumi.

Katika sekta ya afya, Ngajilo aliahidi kusimamia utoaji wa huduma bora bila unyanyasaji, akibainisha kuwa hatakubali kuona wananchi wanateseka hospitalini wakati wanalipa kodi zao.

“Mimi ni mtu wa menejimenti. Nikipewa dhamana, nitahakikisha utoaji wa huduma za afya unakuwa wa viwango. Sitakubaliana na huduma duni au wananchi kunyanyaswa hospitalini. Nitamuomba pia Rais Dk Samia Suluhu Hassan atusaidie kuongeza pia huduma za kibingwa kama moyo na saratani hapa Iringa kwa sababu tupo katikati ya nchi,” alieleza.

Akizungumzia michezo, Ngajilo alisema michezo ni sehemu ya uchumi na ajira kwa vijana, hivyo atahakikisha Iringa inakuwa na timu imara ya ligi kuu na inavutia michezo mikubwa kufanyika mjini humo.

“Michezo ni uchumi. Tunataka timu kubwa zije hapa. Tukipata timu ya ligi kuu, vijana wetu watanufaika na ajira na mzunguko wa pesa utaongezeka,” alisema.

Mwisho.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button