NHIF yaguswa mzigo gharama za matibabu

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umesema kila mwaka unatumia zaidi ya Sh bilioni 700 kugharamia matibabu katika vituo vya kutolea huduma.

NHIF imesema asilimia 60 ya fedha hizo zinatumika kugharamia matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza.

Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa NHIF, James Mlowe amesema hayo alipokutana na kuzungumza na uongozi wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) ukiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TSN, Asha Dachi katika makao makuu ya kampuni hiyo Tazara, Dar es Salaam.

Mlowe alisema kuna ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza katika hospitali nchini na chanzo ni ulaji usiofaa na kutofanya mazoezi.

“Kwa sasa hivi NHIF tupo vizuri kwenye takwimu, katika hizo bilioni 700 tunazolipia matibabu katika vituo vya afya asilimia 60 inalipia hao watu wenye magonjwa yasiyoambukiza zaidi ya Shilingi bilioni 420 kwa mwaka,” alisema.

Mlowe alitaja magonjwa hayo ni kisukari, magonjwa ya moyo, saratani, magonjwa ya figo.

Alisema asilimia 15 ya watu nchini wamejiunga na bima afya na asilimia 85 hawapo katika mfumo wa bima.

Mlowe alisema kwa sasa NHIF ina wagonjwa karibu 2,900 wanaopata huduma ya kusafisha damu kupitia mfuko wa bima na inatumia zaidi ya Sh 3,000,000 kwa mwezi kwa mtu mmoja kugharamia matibabu hayo.

“Sasa hivi mitaani kuna watu wanaishi na pipe (mipira) kila baada ya siku tatu anaenda kusafisha damu, ukienda mara moja unatumia mpaka Sh 350,000, ukienda kama ni mara tatu kwa wiki unatumia zaidi ya 800,000, kwa mwezi unatumia zaidi ya 3,000,000 familia ngapi zinaweza kuhudumia kwa mwezi,” alisema.

Mlowe alisema magonjwa ya moyo, saratani, na kisukarii matibabu yake ni ya gharama kubwa na wananchi wasiokuwa na bima ya afya wengi wanashindwa kumudu.

Alisema kwa sasa NHIF inatoa huduma katika vituo vya afya 10,098 nchi nzima hivyo imesogeza huduma kwa wananchi.

“Kuna dawa za saratani zinauzwa hadi milioni 72 nani anamudu, kuna watu huko mitaani tunajua kabisa huyu tatizo lake ni hili lakini tumeshindwa kumtibu, matibabu yapo lakini ni gharama lakini bima ya afya inasaidia,” alisema Mlowe.

Mlowe alisema ni muhimu wananchi wajiunge na bima ya afya kupitia mpango wa bima ya afya kwa wote ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya na kumudu gharama za matibabu.

Meneja wa NHIF Mkoa wa Temeke, Cannon Luvinga alisema wameboresha zaidi vifurushi vya huduma ili kuhakikisha wananchi wote wanaweza kumudu gharama za matibabu kulingana na kipato chake.

Luvinga alisema kupitia vifurushi vilivyoboreshwa sasa gharama za kujiunga huanzia Sh 120,000 kwa waliopo chini ya miaka 17 kwa mwaka na watu wazima huanzia Sh 167,000.

“Mkurugenzi wetu Mkuu amesaini na kupitisha vifurushi vingine ambavyo vina wigo mpana kutoka viwili sasa vinakua vitano kutakuwa na kifurushi cha chini kinaitwa Tarangile ambacho mtu (0-17) anaweza kujiunga Sh 120,000 na akapata matibabu mwaka mzima,” alisema.

Aliongeza: “Kwa watoto waliopo shule kwa sababu wanakuwa wengi wanaweza kujiunga kwa Sh 50,400,
wengine kuanzia miaka 18-35 anaweza kuingia Sh 167,000 akapata matibabu kwa mwaka”.

Alisema mfuko unaendelea kuboresha mifumo ya utoaji huduma kiteknolojia iliyosaidia kupunguza changamoto za ucheleweshaji wa malipo kwa vituo na kuboresha huduma kwa wateja.

Meneja Rasilimaliwatu wa TSN, Siku Baleja aliomba mfuko huo kuangalia upya vifurushi vyake kwa wafanyakazi wa TSN kutokana na uwepo wa changamoto ya baadhi yao kutopata huduma wanapokwenda kutibiwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa TSN, Asha Dachi alisema TSN ipo tayari kushirikiana na NHIF katika utekelezaji wa
Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote katika kutoa elimu kwa umma.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button