NIC yaja mtaa kwa mtaa

SHIRIKA la Bima la Taifa (NIC) kupitia Mkurugenzi wake wa Masoko na Mawasiliano Karim Meshack amesema wamejipanga kumfikia kila Mtanzania popote pale kupitia kampeni yao ya Mtaa kwa Mtaa.

Akizungumza na HabariLeo  katika Maonesho ya 47 Kimataifa ya Biashara  Saba saba amesema, NIC imedhamiria kutoa elimu kwa wananchi kwa kupita mtaani, ili kuwafikia wananchi wa kada zote kuanzia waendesha bodaboda, bajaji, mama lishe na baba lishe, madereva wa daladala, wafanyabiashara wa sokoni na maeneo mengine.

Amesema tayari wameizindua kampeni hiyo ya elimu katika jijini Mwanza, na itaendelea kufanyika kwa mikoa yote Tanzania bara.

Advertisement

“Watu wanaona bima kama anasa, kama ya matajiri, yakimkuta majanga ha! Nilipaswa kuwa na bima, watu wakiunguliwa kwenye masoko ndio wanakumbuka kuwa walipaswa kuwa na bima, bima ni kumrejesha mtu kwenye hali ya kawaida ya kiuchumi baada ya majanga.” Amesema.

Aidha, Meshack amesema kuwa NIC ipo kwaajili ya kumsaidia mtanzania yeye na mali zake.

“Watanzania wengi wanajenga nyumba kwa kudunduliza kwa miaka mitano mpaka 10,  sasa fikiria nyumba imeungua huna bima uanze kudunduliza tena miaka mitano, 10 utaweza?” amehoji

Hata hivyo amesema “tunatakiwa kuwapelekea elimu hii watanzania ili wajue kukata bima sio anasa, mfano sisi tuna miaka 60 tangu shirika lianzishwe lakini waliokata bima ni asilimia 1.6 ya watanzania wote  milioni 61 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi.

“Tunakazi kubwa sisi pamoja na wadau wengine ya kuhakikisha elimu ya bima inafika kwa watanzania wa kawaida. Tatizo sio fedha, tatizo ni elimu.”Amesisitiza

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *