NIDA yaita makundi manne kubadili taarifa

MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imeita makundi manne yakabadili taarifa zao. Makundi hayo ni walioathirika na vyeti vya shule vilivyoghushiwa wakiwemo waliowahi kufukuzwa katika ajira za serikali kwa kutumia vyeti hivyo na pia waliojisajili NIDA kwa kutumia nyaraka hizo.

Wapo waliotumia majina ya watu wengine kupata vyeti vya elimu, waliotoa taarifa za uongo au udanganyifu wakati wa usajili wa NIDA na raia wa Tanzania ambao waliwahi kujisajili kama wakimbizi. Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, James Kaji amesema NIDA inaita makundi hayo kwa kuwa serikali imetoa kibali kwa ajili ya kushughulikia maombi 18,013 ya mabadiliko ya taarifa zilizowasilishwa kinyume cha sheria na taratibu wakati wa usajili wa vitambulisho vya taifa.

Kaji amesema kibali hicho kinatoa nafasi kwa baadhi ya makundi ambayo awali yalishindwa kufanya marekebisho ya taarifa zao kutokana na kukinzana na miongozo ya usajili na mabadiliko ya taarifa kwenye mfumo wa NIDA. SOMA: Wasiofuata vitambulisho NIDA kusitishiwa namba

“Kibali hiki kimetolewa kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Oktoba 2025, na kitafungwa baada ya ukomo wake kuisha. Ndani ya kipindi hicho, wahusika wanapaswa kufika katika ofisi za NIDA za wilaya na nyaraka sahihi ili kuhuisha taarifa zao,” alisema Kaji

Amesema maombi yatakayofanyiwa kazi ni yale yatakayokidhi masharti na vigezo vilivyowekwa baada ya wahusika kuwasilisha nyaraka zinazotakiwa kwa ajili ya kuthibitisha taarifa zao. “Nachukua fursa hii kuwataka wananchi wa makundi hayo manne, kufika katika ofisi za NIDA za wilaya wakiwa na nyaraka zinazohitajika ikiwemo cheti cha ubatizo, vyeti vya elimu, cheti cha kuzaliwa ikitegemea na changamoto iliyopo, kushughulikia maombi ya mabadiliko hayo,” alisema Kija.

Amesema katika Serikali ya Awamu ya Tano watu zaidi ya 18,000 ambao walifukuzwa kazi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo walioghushi vyeti walipata msamaha wa kurudi na kupokea pensheni zao lakini changamoto imekuja upande wa NIDA. “Nasi tunatoa msamaha huu, hakuna atakayeshitakiwa, jitokezeni mpate huduma,” alisema Kija.

Ametoa wito kwa jamii itoe taarifa sahihi wanapofika kwenye ofisi za NIDA ili kuepuka usumbufu usio wa lazima na kudai kuwa wamezuia vitambulisho 600 eneo la Horohoro baada ya kufuatilia na kugundua kuwa wanaohitaji vitambulisho si raia wa Tanzania. Kuhusu waliopoteza vitambulisho kuambiwa kujaza fomu upya, Kija alisema ni lazima mhusika ajaze fomu ili kujiridhisha kama kweli taarifa za awali na za wakati huu (sasa) ni sawa au zina mabadiliko ili kuepuka kujirudia makosa ya awali

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button