NIDA yatoa maelekezo wasiopata vitambulisho Kigoma
KIGOMA; MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) mkoa Kigoma, imewataka wananchi wa mkoa huo kujitokeza kuchukua vitambulisho vyao kutokana na idadi kubwa ya vitambulisho kutengenezwa, lakini ni idadi ndogo ya watu wanaojitokeza kuchukua vitambulisho hivyo.
Ofisa wa NIDA Mkoa Kigoma, Odoyo Albertus amesema hayo mjini Kigoma akitoa maelezo kwa wajumbe wa Baraza la Biashara la Mkoa Kigoma, ambalo lilikuwa likijadili ajenda ya kutopatikana vitambulisho vya Taifa kuathiri biashara za wajasiriamali kufanya biashara za kuvuka mpaka.
Albertus alisema kuwa zaidi ya vitambulisho 250,000 vimeletwa mkoani Kigoma kwa ajili ya kugawiwa vikielekezwa kwenye ofisi za watendaji wa kata na kwamba wananchi wote wametakiwa kwenda kwenye ofisi za watendaji wa kata kuchukua vitambulisho vyao.
Akizungumzia malalamiko ya waliohojiwa kutopata vitambulisho, alisema kuwa mkoa ulipokea majina ya watu 255,000 waliokuwa na changamoto mbalimbali kubwa, ikiwa ya uraia na kutakiwa kurudi tena kufanyiwa uhakiki, lakini ni watu 41,000 waliorudi na kuhakikiwa huku wengine wakiitangaza NIDA vibaya kwamba ina usumbufu kupata vitambulisho.
Akizungumza kwenye mkutano huo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa Kigoma, Juma Chaurembo alisema kuwa kumekuwa na usumbufu mkubwa wa upatikanaji wa vitambulisho hivyo, jambo linalofanya watu wengi kukata tamaa kufuatilia vitambulisho hivyo.
Naye Mkuu wa mkoa Kigoma, Thobias Andengenye amewataka wananchi wa mkoa Kigoma kujitokeza kwenye ofisi za watendaji wa kata kuchukua vitambulisho vyao na wenye changamoto wafuate taratibu za kushughulikia changamoto hizo.