NIMR yaja na utafiti wenye virusi vya Ukimwi, kisukari

DODOMA; TAASISI ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), imeendelea na utafiti wa kuzuia ugonjwa wa kisukari, ambapo tafiti hizi zimeonesha kuwa wagonjwa wenye virusi vya UKIMWI wapo katika hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa kisukari.
Kauli hiyo imetolewa bungeni mjini Dodoma leo na Waziri wa Afya, Jenista Mhagama alipokuwa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Wizara ya Afya kwa mwaka 2025/2026.
“ Aidha, taasisi inafanya utafiti wa jaribio nasibu la awamu ya tatu ili kuangalia ikiwa matumizi ya dawa ya Metformin kwa watu wenye virusi vya UKIMWI wenye dalili za awali sana za kisukari yanaweza kupunguza uwezekano wa watu hawa kupata ugonjwa wa kisukari. Jaribio hilo linafanyika katika Mkoa wa Dar es Salaam.
“Washiriki 1,634 wameandikishwa na ufuatiliaji utafanyika kwa miaka minne (4) ili kuweza kujua ikiwa dawa hii inasaidia kukinga watu kupata ugonjwa wa kisukari,” amesema Waziri Mhagama.