Nishati ya umeme jua kupunguza hewa ukaa sekta ya uvuvi

TAASISI ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), imeanza kufanya utafiti utakaozuia au kuepusha wachakataji wa mazao ya uvuvi ikiwemo dagaa na samaki, kutumia kuni au kukata mikoko kuchemsha dagaa na badala yake watumie nishati mbadala.
Mkurugenzi Mkuu wa TAFIRI, Dk Ismael Kimirei ameyasema hayo leo Dar es Salaam katika kongamano na maonyesho ya tisa ya Sayansi Teknolojia na Ubunifu yaliyoandaliwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH).
Dk Kimirei amesema wamepata fedha kutoka COSTECH kwa ajili ya kufanya utafiti huo na kwamba wanalenga kuwezesha wachakataji kutumia nishati ya umeme jua kukausha samaki au dagaa hata kunapotea mabadiliko ya hali ya hewa.
Amesema watatengeneza mabanda yatakayotumia nishati hiyo hivyo, watapunguza utegemezi kwenye kuni kwenye kukausha samaki na dagaa.
“Ziwa tanganyika tumeweka majiko banifu kwa ajili ya kukausha dagaa na samaki kwa kutumia kuni chache,” ameeleza Dk Kimirei.
Ameongeza kuwa utafiti huo unajielekeza katika kupunguza matumizi ya hewa ukaa yanayotokana na matumizi ya kuni na taa za mafuta wakati wa uvuvi.
“Katika utafiti tuliofanya tumebaini upotevu mkubwa wa dagaa kwa asilimia 40 inamaana kuwa ukivua kilogramu 100 za dagaa kilogramu 40 hazifiki mezani kwako, zinapotea,” amesema.
Hivyo, katika mkakati wa kupunguza upotevu huo wa mwaka 2023-2030 wanalenga kupunguza upotevu kwa asilimia 60 ili chakula hicho kiweze kuwafikia walaji.
Katika kutekeleza mkakati huo, wanahitaji kuwekeza katika mnyororo wa ubaridi ili wavuvi wanapofika mwaloni, samaki au dagaa wawe safi.
“Tayari Rais Samia Suluhu Hassan ameanza kutekeleza mkakati huu kwa kutoa maboti kwa ajili ya uvuvi na yana maeneo ya kuhifadhi kwa ubaridi kwa upande wa baharini, lakini Bado uwekezaji zaidi unahitajika,” amesema.
Pia amesema wanahitaji miundombinu ya utunzaji wa mazao hayo ya uvuvi, kuongeza thamani na kuhifadhi.
“Pamoja na mabadiliko ya tabia nchi tuliyonayo, tunahitaji kuwekeza katika kuongeza ubora na ubunifu ili kiasi cha samaki kinachovuliwa kiokolewe kwa kiasi kikubwa na hewa ukaa ipungue kwa kiwango kikubwa,” amesisitiza.
Dk Kimerei amesema kuwa mabadiliko ya tabia nchi yanaathiri sekta zote za uchumi ikiwemo sekta ya uvuvi.
Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika yaliwahi kujaa na maji kuitiliza kwenye eneo lake la asili na ili kuzuia lazima wazuie kutokea nchi kavu.
Amesema mabadiliko ya tabia nchi yanaigusa sekta ya uvuvi kwani kuna watu wanaoongeza thamani kwa kuoka au kukausha mazao ya uvuvi kama vile samaki na dagaa.



