NIT yajipanga ujenzi, usanifu wa meli

CHUO cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kimeingia makubaliano na Kampuni ya Dar es Salaam Merchant Group (DMG) ili kuzalisha wataalamu wabobezi katika sekta ya usafiri na usafirishaji hususani kwenye eneo la ujenzi na usanifu wa meli.

Wakizungumza mara baada ya kusaini makubaliano hayo juzi Dar es Salaam, Mkuu wa NIT, Profesa Zacharia Mganilwa na Mkurugenzi Mkuu wa DMG, Rayton Kwembe walisema makubaliano hayo yatasaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha taaluma katika eneo la uchumi wa buluu.

Profesa Mganilwa alisema kupitia makubaliano hayo, DMG itatoa mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa NIT, hivyo kuhitimu kama wataalamu wabobezi kwenye sekta nyeti ya usafiri na usafirishaji.

Advertisement

“Madhumuni makuu ya makubaliano haya ni kuimarisha uhusiano kati ya NIT na DMG katika kuboresha ujuzi kwa wanafunzi na wafanyakazi katika maeneo ya usafiri wa maji,” alisema na kuongeza:

“Tumeingia makubaliano katika maeneo kadhaa ambapo mojawapo ni mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi, mafunzo kwa wafanyakazi, kubadilishana utaalamu, ziara za mafunzo ama masomo na vilevile kukuza uhusiano kwa wafanyakazi.”

Aliyataja maeneo mengine ya ushirikiano katika mkataba huo kuwa ni utafiti na ushauri na kusisitiza: ‘Wataalamu kutoka DMG wataweza vilevile kushiriki katika programu za mafunzo katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji.’

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa DMG alisema: “Katika makubaliano haya, kampuni yetu imekubali kutoa nafasi za mafunzo kwa vitendo ikiwa ni pamoja na kutoa fursa ya ziara za masomo na uhusiano kwa wafanyakazi na wanafunzi.”

Makubaliano hayo yatadumu kwa kipindi cha miaka mitano ambapo wanafunzi na wakufunzi kutoka NIT watapata fursa ya kujifunza ujenzi wa meli pamoja na ukarabati wake.

Alisema hivi sasa nchi haina wataalamu wa kutosha katika ujenzi na ukarabati wa meli ambapo imefanya wengi wa wataalamu hao kuchukuliwa Korea na China.

Alisisitiza kuwa kwa kupitia makubaliano hayo, ana imani kuwa kwa miaka michache ijayo, taifa litakuwa na wataalamu wengi wabobezi kwenye eneo hilo.

“Tunataka kuona miradi mingi ya ujenzi na ukarabati wa meli inasimamiwa na Watanzania, hivyo tutaweka juhudi kubwa kuhakikisha mkataba huu tulioingia unakuwa wenye tija kwetu sote na taifa kwa ujumla,” alisema.

Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa kampuni yao inatoa zawadi kwa wanafunzi wa chuo hicho wanaofanya vizuri katika masomo yao na vilevile kuwapa ajira wahitimu hao.

Hata hivyo, Mkuu wa NIT alisema kuwa makubaliano ambayo chuo chake wameingia na kampuni hiyo ni sehemu ya kutimiza malengo ya Mradi wa Kujenga Ujuzi kwa Maendeleo na Uingiliano wa Kikanda katika Afrika Mashariki (EASTRIP).

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *