Norway yaipongeza Tanzania udhibiti wa rasilimali

DAR ES SALAAM: WAZIRI Mkuu wa zamani wa Norway, Helen Clark ambaye pia ni Mwenyekiti wa Asasi ya Bodi ya Kimataifa ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia (EITI) ya Norway, ameipongeza Tanzania kwa usimamizi madhubuti wa rasilimali hizo muhimu.

Amesema hayo leo jijini Dar es Salaam, alipofanya kikao na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko kwenye ofisi ndogo za Wizara ya Nishati.

Katika kikao hicho, Dk Biteko amesema kuwa, Tanzania inaimarisha usimamizi wa rasilimali hizo ili kufikia viwango vya ubora wa kimataifa pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya EITI na Taasisi inayosimamia rasilimali hizo nchini (TEITI).

Advertisement

Kwa upande wake Clark amesema, ziara hiyo ni hatua muhimu katika kuimarisha usimamizi wa rasilimali hizo hapa nchini ili kufikia viwango vya ubora wa kimataifa unaotakiwa katika usimamizi wa rasilimali pamoja na kuimarisha ushirikiano baina ya EITI na TEITI.

Mbali na majadiliano ya kiserikali, Helen Clark pia atakutana na wadau mbalimbali wanaohusika katika sekta hiyo nchini kwa lengo la kujadiliana kuhusu changamoto na fursa za utekelezaji wa kanuni na taratibu za EITI, kujadili njia bora ya pamoja katika kuhamasisha uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali hizo.

Matarajio ya ziara hiyo ni kuisaidia Tanzania kuimarisha usimamizi bora wa rasilimali zake za madini, mafuta pamoja na gesi asilia sambamba na kuisaidia Tanzania kufikia viwango vya kimataifa katika usimamizi wa uwazi na uwajibikaji na kuendelea kuwa mfano kwa mataifa mengine katika usimamizi wa rasilimali hizo.