Nyamka ateuliwa Kamishna Jenerali Magereza

RAIS Samia Suluhu Hassan amemteua Kaimu Kamishna wa Magereza Huduma za Urekebishaji, Mzee Nyamka kuwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza (CGP).

Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu kwa vyombo vya habari Ijumaa, ilisema uteuzi huo wa Nyamka umeanza Agosti 24, mwaka huu.

Nyamka anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Meja Jenerali Suleiman Mzee ambaye hivi karibuni aliteuliwa na Rais Samia kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara.

Anakuwa Kamishna Jenerali wa Magereza wa tano ndani ya miaka 10 akitanguliwa na Joan Minja (2012 – 2017), Dk Juma Malewa (2017 – 2018), Phaustine Kasike (2018 – 2020) na Suleimani Mzee (2020 – 2022).

Wasifu wake

Kwa mujibu wa taarifa ya Kitengo cha Habari na Mawasiliano, Makao Makuu ya Jeshi la Magereza, Msalato Dodoma, kwa vyombo vya habari jana, Kamishna Jenerali mteule Nyamka ni mbobezi katika masuala ya fedha na aliwahi kuhudhuria mafunzo mbalimbali ya fani hiyo.

Mafunzo hayo ni ya uhasibu wa sekta za umma, mafunzo ya mifumo jumuishi ya usimamizi wa fedha na mafunzo ya kugundua na kuzuia udanganyifu.

Taarifa hiyo ilibainisha kuwa Nyamka alizaliwa mwaka 1964 Wilaya ya Tanga Mjini mkoani Tanga na kusoma katika Shule ya Msingi Muhimbili, Dar es Salaam mwaka 1973 hadi 1979 na alihitimu sekondari katika Shule ya Sekondari Mzizima mkoani Dar es Salaam mwaka 1983.

Pia Oktoba 1995 kabla ya kujiunga na Jeshi la Magereza, alihamia Makao Makuu ya Magereza akitokea Wizara ya Fedha akiwa mtumishi raia na Januari Mosi, 1996 alijiunga rasmi na jeshi hilo kwa kuhudhuria mafunzo ya Uongozi Daraja la Kwanza katika Chuo cha Maofisa Magereza Ukonga na kuhitimu mafunzo hayo Mei 31, 1996.

Alipata Stashahada ya Juu ya Uhasibu katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) Dar es Salaam mwaka 1995 na mwaka 2004 alitunukiwa Stashahada ya Uzamili ya uhasibu chuoni hapo.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa katika utumishi wake ndani ya Jeshi la Magereza, amepandishwa vyeo mbalimbali ikiwamo Mkaguzi Msaidizi wa Magereza (1996-2001), Mkaguzi wa Magereza (2001-2005), Mrakibu Msaidizi wa Magereza (2005-2009), Mrakibu wa Magereza (2009-2011) na Mrakibu Mwandamizi wa Magereza (2011-2013).

Vyeo vingine ni Kamishna Msaidizi wa Magereza (2013-2017), Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza 2017 hadi anapata uteuzi wa CGP.

Aidha, aliwahi kufanya kazi katika nafasi ya Mkufunzi katika Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania (TCTA) mwaka 2001-2005, Mhasibu wa Magereza Mkoa wa Iringa 2005-2009, Mkufunzi katika Chuo cha TCTA 2009 – 2011 na Mkuu wa Sehemu ya Hoja na Ufungaji Mahesabu 2012 – 2014.

Nyamka pia alikuwa Ofisa Mnadhimu Magereza Pwani (2014-2015), Ofisa Mnadhimu Magereza Mkoa wa Morogoro (2015-2017, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Morogoro (2017 – 2018), Ofisa Mnadhimu Jeshi la Magereza (2018-2021), Kaimu Kamishna Huduma za Urekebishaji Jeshi la Magereza 2021 hadi anapata uteuzi wa CGP.

 

 

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button