Nyumba 865 kuunganishwa gesi Mtwara, serikali kugawa mitungi ya ruzuku

NAIBU Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) inatarajia kuunganisha mfumo wa gesi ya kupikia kwa takribani nyumba 865 mkoani Mtwara, katika maeneo yenye miundombinu ya bomba la gesi.

Kapinga amesema hayo leo, Mei 13, 2025, bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Tunza Malipo, aliyetaka kufahamu mkakati wa serikali wa kuunganisha gesi kwa taasisi na nyumba za wananchi mkoani humo.

“Katika Mkoa wa Mtwara, Serikali imeshapeleka miundombinu ya usambazaji wa gesi asilia katika baadhi ya maeneo na jumla ya nyumba 425 pamoja na taasisi nne zimeunganishwa na mtandao wa matumizi ya gesi asilia katika maeneo ya Mtwara Mjini,” amesema Kapinga.

Ameongeza kuwa kwa sasa usanifu wa kihandisi kwa ajili ya kuunganisha nyumba 865 umekamilika na hatua inayofuata ni utekelezaji wa mradi huo.

Aidha, amesema tayari Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko, ameshauagiza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na TPDC kushirikiana ili kuongeza kasi ya uunganishaji wa gesi asilia kwa wananchi wa Mtwara na Lindi.

Akijibu swali la Mbunge wa Temeke, Dorothy Kilave kuhusu umuhimu wa kuharakisha uunganishaji wa gesi katika masoko ya Sterio, Temeke, Keko na Mtoni kwa ajili ya Mama Lishe na Baba Lishe, Kapinga amesema Serikali kupitia TPDC ina mkakati wa kuunganisha gesi katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, na masoko hayo tayari yamechukuliwa kwa ajili ya kufanyiwa tathmini.

Kwa upande wake, Mbunge wa Momba, Kondesta Sichwale, alihoji kuhusu idadi ndogo ya wananchi wanaofikiwa na mitungi ya gesi ya ruzuku, na kupendekeza mitungi hiyo isambazwe kupitia kwa watendaji wa Kata ili wananchi wachukue kwa kutumia vitambulisho vyao vya NIDA.

Akijibu hoja hiyo, Kapinga amesema kuwa Serikali inaanza kugawa mitungi ya gesi ya ruzuku takribani 420,000. Amesema utaratibu uliowekwa ni kwa kila mwananchi kuchukua mtungi mmoja kwa kutumia namba yake ya NIDA ili kuhakikisha ufanisi na uwiano katika ugawaji huo.

Ameongeza kuwa Serikali imetenga mitungi 3,255 kwa kila wilaya kama hatua ya mwanzo ya utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia. Kapinga amewahakikishia Wabunge kuwa mkakati huo ni wa muda mrefu wa miaka kumi na unalenga kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwisho wa kipindi hicho, sambamba na maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

Habari Zifananazo

3 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button