Ombi la Lissu latekelezwa Chadema

DAR ES SALAAM; KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) John Mnyika amesema chama hicho kimezialika taasisi za kimataifa na taasisi za kidini kushuhudia uchaguzi mkuu wa chama hicho ili kuhakikisha unakuwa wa uhuru na haki.

Januari Mosi mwaka huu, mgombea wa nafasi ya mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu wakati akitoa salamu za mwaka mpya, alitoa mapendekezo kwa kamati kuu kuwaalika viongozi wa madhehebu ya dini pamoja na wawakilishi wa mabalozi kushiriki kama watazamaji wa uchaguzi huo ili kuepuka mianya ya udanganyifu.

Mnyika alisema hayo jana akizungumza na wanahabari katika makao makuu ya chama hicho mkoani Dar es Salaam.

Akizungumzia juu ya watazamaji wa uchaguzi huo, alisema taasisi za kimataifa, taasisi za ndani na taasisi za kidini zitakuwepo kufuatilia ili uwe wa huru na haki.

“Katika mkutano huu wa chama, tumealika taasisi mbalimbali kama ulivyo utaratibu wetu wa siku zote wa Chadema, taasisi za kimataifa taasisi za ndani ya nchi taasisi za kiimani kwa maana za kidini watakuja kushuhudia ufunguzi wetu na taratibu nyingine,” alisema Mnyika.

Alisema kanuni za kikatiba za chama zinawataka wajumbe pekee kushiriki katika uchaguzi huo.

“Katika vikao vya uchaguzi, wajumbe halali wa kikatiba ndio wataruhusiwa kupiga kura katika uchaguzi, wawakilishi wa wajumbe wa kikatiba kama watakuwepo watatakiwa watoke nje ya ukumbi wakati wa kupiga kura,” alisema Mnyika akirejelea kanuni za chama hicho.

Mnyika pia amesema chama hicho kimeweka utaratibu kwa vyombo vya habari kuwepo katika ukumbi wa kupigia kura ili kuwepo na uwazi

“Tutaweka mazingira katika ukumbi wa uchaguzi ambayo yataruhusu vyombo vya habari pamoja na kuwa si wajumbe wa kikatiba kuwepo kushughulikia masuala ya uchaguzi,” alisema.

Akizungumzia uchaguzi huo, alisema wagombea 300 wamechukua fomu kwa ajili ya kugombea nafasi za uongozi katika mabaraza mbalimbali ya chama hicho.

Aliwataka wagombea hao kuzingatia kanuni, taratibu, miongozo pamoja na katiba ya chama kuelekea uchaguzi huo.

Aidha, Mnyika alisema baada ya kurejesha fomu, hatua inayofuata ni usaili na uteuzi wa wagombea wa mabaraza ya chama utakaoanza Januari 10 hadi 11 mwaka huu.

Kwa upande wa baraza la wazee, wapo wagombea 85, baraza la vijana wagombea ni 66 na baraza la wanawake lina wagombea 93.

Katika hatua nyingine, Mnyika amewataka wagombea wenye mapendekezo kufuata taratibu za uwasilishaji wake.

“Ili chama kiweze kushughulika na mapendekezo na kisiache mapendekezo na kuonekana kinachukua wazo la huyu na kuacha la yule, mgombea yeyote mwenye mapendekezo ambayo hayapo humu kwenye kanuni zetu za chama ambayo yanatekelezeka, aandike barua rasmi kwa katibu mkuu wa chama kuainisha mapendekezo yake,” alisema.

Aliongeza: “Mpaka nazungumza nanyi hapa, sijapokea barua ya mgombea yeyote akitoa pendekezo lolote kuhusiana na utaratibu wa uendeshaji wa uchaguzi.”

 

Habari Zifananazo

Back to top button