DODOMA : WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo amesema tangu kuanzishwa kwa mradi wa usafiri wa reli ya kisasa (SGR) serikali imezalisha ajira za watu zaidi ya 30,176 za moja kwa moja na 150,000 zisizo za moja kwa moja.
Akiwasilisha mapendekezo ya mpango wa maendeleo kwa mwaka wa fedha 2024/2025 bungeni mjini Dodoma, Prof. Mkumbo amesema ongezeko hili la ajira limechangia serikali kuingiza mapato ya shilingi bilioni 358.74.
Prof. Mkumbo amesema fursa nyingine ambazo zimepatikana ni viwanda wazabuni na wakandarasi ambapo hadi sasa jumla ya kampuni 2,460 zinashiriki katika mradi huo zenye thamani ya shilingi trilioni 3.69.
Hatahivyo amesema mradi wa SGR unaendelea kuchochea kwa kasi ongezeko la mahitaji ya saruji na vifaa vya ujenzi na kuifanya sekta ya viwanda kuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi
“Ukiangalia tu muda wa safari kati ya Dar es Salaam na Dodoma kutoka wastani wa masaa kumi kwa basi hadi masaa matatu hii ni faraja kubwa kwa wananchi’, alisema Profesa Mkumbo.
Aliongezea,“tangu kuanza kwa safari za (SGR) abiria waliosafiri tu walikuwa 645,421 ambapo serikali imeingiza shilingi bilioni 15.695”, alisema Prof. Mkumbo.
Katika suala la utunzaji wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,Waziri Mkumbo amesema mradi wa usafiri wa reli ya kisasa (SGR) umesaidia kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa hasa ukizingatia treni hizi zinatumia nishati ya umeme.
Waziri Mkumbo amesema mradi wa usafiri wa reli ya kisasa (SGR) umeweza kuongeza kipato cha serikali kutokana na ongezeko kubwa la abiria ma kuongeza tija katika shughuli za utalii hasa katika maeneo yanayopita ikiwemo Hifadhi ya Mikumi na Hifadhi ya Ruaha (kupitia Stesheni ya Kilosa), Hifadhi ya Katavi (Stesheni ya Tabora), Hifadhi ya Gombe (Stesheni ya Kigoma), na Hifadhi ya Serengeri (kupitia Stesheni za Malampaka na Mwanza).
Profesa Mkumbo amesema ukamilishaji wa mradi wa usafiri wa reli ya kisasa (SGR) utaweza kusaidia Tanzania kuongeza ufanyaji wa biashara na kuongeza fursa za uwekezaji ndani na nje ya nchi.
“hadi kufikia Septemba 2024 jumla ya miradi 519 imesajiliwa na Kituo cha Uwekezaji (TIC) katika ushoroba wa reli yenye kuvutia mtaji wa dola za kimarekani 4.59 bilioni na kutarajia kuzalisha ajira 115,566”,alisisitiza Prof. Mkumbo.